Daily Archives: August 6, 2014

MAONO HASI YANAIPOTOSHA SEKTA BINAFSI YA MAREKANI KUHUSU AFRIKA – RAIS KIKWETE

 

 Jakaya-Kikwete

 Maono hasi yanaipotosha sekta binafsi ya Marekani kuhusu Afrika – Rais Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka sekta binafsi na wafanyabiashara wa Marekani kujifunza kutoka kwa wenzao wa Bara la Asia, ambao wameongeza uwekezaji wao katika Afrika kwa sababu wanapata habari sahihi na za kweli kuhusu Afrika kutoka kwa vyombo vyao vya habari.

Aidha, Rais Kikwete  amesema kuwa pingamizi kubwa la kufanya biashara kati ya Marekani na Afrika siyo tena Bahari ya Atlantic ama umbali bali ni maono hasi yanayojengwa na vyombo vya habari vya Marekani kuhusu Bara la Afrika.

Rais Kikwete ameyasema hayo jana, Jumatatu, Agosti 4, 2014 wakati wa sherehe ya kuwekwa kwa Rais Kikwete katika Jumba la Mashujaa wa Uongozi wa Afrika la Jarida la African Leadership – African Leadership Hall of Fame – kwenye Jengo la National Press Club mjini Washington, D.C., Marekani ambako Rais anafanya ziara ya siku tisa.

Sherehe hiyo ya kumwingiza Rais Kikwete kwenye Africa Leaderrship Hall of Fame imefanyika wakati wa Chakula cha Mchana cha 5th African Business Leadership Award Luncheon kwenye Jumba hilo la National Press Club.

Rais Kikwete anakuwa kiongozi wa tatu wa Afrika kutunukiwa heshima hiyo kubwa. Marais waliotangulia kupewa heshima hiyo ni Rais wa Sierra Leone na Rais wa Namibia.

Akizungumza kabla ya kukabidhiwa medali na cheti cha kutunukiwa heshima hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa vyombo vya habari havijali sana maendeleo mazuri ya Bara la Afrika. “Matokeo yake ni kwamba sekta binafsi ya Marekani imefanywa kuamini kuwa Bara la Afrika ni bara hatari sana kuwekeza.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Mara nyingi, Afrika inaonekana kama nchi moja badala ya Bara moja, na hivyo tatizo katika nchi moja kwa urahisi sana linafanywa tatizo la nchi zote na kwa namna hasi. Hii ni tofauti na Bara la Asia, ambako vyombo vya habari huelezea picha nzuri za matukio ya Afrika. Hii ndiyo maana kuna ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi ya Asia katika Afrika leo kuliko ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.”

Rais Kikwete ameongeza: “Hivyo, pingamizi kubwa ya kufanya biashara kati ya Afrika na Marekani siyo Bahari ya Atlantic wala umbali kati ya maeneo hayo. Pingamizi ni maono hasi. Tunayo kila sababu ya kumshukuru Rais Obama kwa uongozi wake na dhamira yake kubadilisha gurudumu hili la historia.”

Ameongeza: “Uamuzi wake kuitisha Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na kuiwekea Sekta Binafsi ya Marekani ushiriki muhimu katika Mkutano huo ni uamuzi wa kimapinduzi. Afrika imekuwa inasubiri fursa hii ya kufanya biashara na Marekani kwa muda mrefu. Na tumedhamiria kutumia fursa hii kwa kadri inavyowezekana.”

Rais Kikwete amelishukuru Jarida la The African Leadership kwa mchango wake mkubwa wa kujenga uhusiano kati ya Afrika na Marekani.

Aidha, Rais Kikwete amelishukuru Jarida hilo kwa kumtunuku tuzo ya Kiongozi Bora wa Kusukuma Maendeleo Mwaka 2013 – The Most Impactful African Leader of the Year Award 2013, tuzo ambayo Rais Kikwete alipewa Aprili 9, 2014. Tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba ya Rais Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe.

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu – Dar es Salaam.

05 Agosti, 2014