Daily Archives: June 13, 2020

Taarifa kwa vyombo vya Habari

                             TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ikulu, Chamwino.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amezungumza kwa njia ya simu na Rais Mteule wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye na kumpongeza kwa uamuzi wa Mahakama ya Katiba nchini Burundi iliyoagiza Rais Mteule aapishwe haraka.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Rais Magufuli amemtakia heri Mhe. Rais Mteule Ndayishimiye kuelekea kuapishwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Burundi kutakakofanyika hivi karibuni.

Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Mhe. Rais Mteule Ndayishimiye kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake wa karibu na Burundi kwa kuwa nchi hizo ni majirani, marafiki na ndugu wa kihistoria.

Mhe. Rais Magufuli amerudia kumpa pole kwa msiba wa kuondokewa na Rais wa nchi hiyo, Mhe. Pierre Nkurunziza aliyefariki dunia tarehe 09 Juni, 2020 na amemueleza kuwa yeye na Watanzania wote wanaungana na Warundi katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Amemuomba kufikisha salamu zake za rambirambi kwa Warundi wote na kuwasihi waendelee kuwa watulivu na wastahimilivu.

KUMBUKUMBU;   Rais Magufuli alipokutana na Rais Mteule wa Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye  wakati huo akiwa Mjumbe Maalum  wa Rais Burundi mwaka 2017. Ikulu jijini Dar es salaam