Daily Archives: June 29, 2020

Taarifa kwa vyombo vya Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Juni, 2020 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mahandaki 4 ya milima inamopita reli ya kisasa (standard gauge) likiwemo handaki refu kuliko yote hapa nchini na ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Kilosa – Rudewa Mkoani Morogoro.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi la miradi hiyo miwili zimefanyika katika eneo la Mkadage Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, lilipojengwa handaki lenye urefu wa kilometa 1.1 ambalo linakua handaki la reli refu kuliko yote hapa nchini na ni moja ya mahandaki 4 yenye jumla ya urefu wa kilometa 2.7 katika mradi wa ujenzi wa reli hiyo kuanzia Dar es Salaam hadi Makutupora Mkoani Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakandarasi na Wakuu wa Mikoa ya Morogoro na Dodoma amelikagua handaki hilo kwa miguu umbali wa zaidi ya kilometa 1 na ametia saini katika ukuta wa lango la handaki hilo.
Mahandaki hayo yanachimbwa ili kuwezesha treni kukwepa milima na mito ukiwemo mto Mkondoa ulio kando ya handaki refu la Mkadage ambalo litaunganishwa na daraja refu meta 487 la kuvuka mto huo.
Barabara iliyowekwa jiwe la msingi ni ya Kilosa – Rudewa yenye urefu wa kilometa 24 ambayo ujenzi wake unafanywa na muungano wa kampuni za ukandarasi za Tanzania kwa gharama ya shilingi Bilioni 33.4. Barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Dumila – Kilosa – Mikumi ambayo inapita nje ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na katika maeneo ya uzalishaji wa mazao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mkadage, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na kazi nzuri ya utoboaji wa milima ili kupata mahandaki hayo, lakini ameelezea kutofurahishwa na ujenzi wa barabara ya Kilosa – Rudewa na hivyo ametoa mwezi mmoja kwa kazi hiyo kuanza kwa kasi inayotakiwa, vinginevyo wakandarasi watafukuzwa na viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano watawajibishwa
Amewataka Watanzania wote kutembea kifua mbele kwa mafanikio makubwa ya ujenzi wa reli ya kati kwa sehemu ya kuanzia Dar es Salaam – Morogoro – Makutupora ambayo ujenzi wake utagharimu shilingi Trlioni 7.026 na miradi mingine mikubwa ukiwemo Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 kwa gharama ya zaidi ya shilingi Trilioni 6 na kuhamisha Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Makao Makuu Dodoma kwa kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa fedha za Watanzania wenyewe.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania hasa waliopo karibu na maeneo ya utekelezaji wa miradi hiyo kuchangamkia fursa mbalimbali za kujipatia kipato na kuongeza uzalishaji mali ikiwemo kulima mazao na kuanzisha shoroba za uzalishaji.
Kuhusu maombi ya ujenzi wa barabara za lami, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kilosa – Mikumi yenye urefu wa kilometa 70 na barabara ya Ifakara – Malinyi – Londo.
Akiwa njiani kuelekea Mkadage, Mhe. Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Kijiji cha Kimamba wamelalamikia kitendo cha mwekezaji ambaye sio raia wa Tanzania kumilikishwa shamba la ekari 5,000 ilihali wao wanakosa mashamba ya kulima. Kutokana na malalamiko hayo, Mhe. Rais Magufuli ameagiza hati za shamba hilo pamoja na mashamba mengine 49 ziwasilishwe Ikulu ndani ya siku 7 ili zifutwe na mashamba kugawiwe kwa wakulima
Na akiwa njiani kutoka Mkadage, Mhe. Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Kijiji cha Ilonda Wilayani Kilosa ambao wamelalamikia kitendo cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Bw. Asajile Mwambambale kuidhinisha mwekezaji Swai Frank Palilo aachiwe shamba lenye ukubwa wa ekari 1,200 hata kabla Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi hajatoa maamuzi baada ya timu aliyounda kushughulikia mgogoro wa shamba hilo kuwasilisha ripoti ya uchunguzi kwake.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaonya viongozi wa Wilaya ya Kilosa kwa kutoshughulikia kero mbalimbali za wananchi ipasavyo hususani migogoro ya ardhi, akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ambaye amewaomba radhi wananchi wa Kijiji cha Ilonga na Mhe. Rais kwa kuidhinisha shamba kubwa aatiwe mwekezaji mmoja ilihali wananchi wanakosa mahali pa kulima.
Mhe. Rais Magufuli amerejea Chamwino Mkoani Dodoma akitokea Mkoani Morogoro alikokuwa katika ziara ya kikazi ya siku 2.