Daily Archives: July 6, 2020

Taarifa kwa vyombo vya Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 06 Julai, 2020 amewaapisha Wakuu wa Mikoa 2, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya 1 na Katibu Tawala wa Mkoa 1, na pia ameshuhudia Wakuu wa Mikoa wakiwaapisha Wakuu wa Wilaya 9 Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma.

Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Kamishna wa Polisi Thobias Emir Andengenye kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Philemon Rugumiliza Sengati kuwa Mkuu wa Mkoa Tabora, Bw. James Wilbert Kaji kuwa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Bi. Mariam Perla Mmbaga kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia kuapishwa kwa Kanali Mathias Julius Kahabi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Ismail Twahir Mlawa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Bw. Albinus Mgonya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Bw. Wilson Samwel Negile Shimo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale na Bw. Abbas Juma Kayanda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu.

Wengine aliowashuhudia wakiapishwa ni Bw. Toba Alnason Nguvila kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhandisi Martine Ntemo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Bw. Lazaro Jacob Twange kuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati, Bi. Jamila Yusuph Kimaro kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda na Bw. Salum Abdallah Kalli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu.

Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhuriwa na Wakurugenzi wa Halmashauri walioteuliwa hivi karibuni ambao ni Bw. Elias Amede Ng’wanidako (Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya), Anastazia Tutuba (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same), Bw. Saad Mutambule (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha), Bw. Duncan Golden Thebas (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala) na Bw. Mwailafu Thomas Edwin (Mkurugenzi wa Mji wa Nanyamba).

Wengine ni Bi. Erica Epaphras Yegella (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara), Bw. Hassan Njama Hassan (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero), Bw. Kanyala Malima Mahinda (Mkurugenzi Mtendaji wa Mji wa Ifakara) na Bw. Waziri Khachi Kombo (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo).

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi wote walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali walizopangiwa na amewataka kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia viapo vyao, taratibu na sheria na kushughulikia kero za wananchi, badala ya kuacha kero hizo zikisubiri kushughulikiwa na viongozi wa kitaifa.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. James Wilbert Kaji aliyekuwa Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na ameamua kumthibitisha kushika wadhifa huo kutokana na utendaji wake mzuri ambapo hivi karibuni alifanya operesheni katika Mkoa wa Arusha na kufanikiwa kukamata magunia 143 (sawa na tani 2.5) za bangi.

Pamoja na kumthibitisha Bw. Kaji, Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua dhidi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Afisa Usalama wa Wilaya (DSO) na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OCCID) katika Mkoa wa Arusha ambako operesheni iliyoongozwa na Kamishna Jenerali Kaji imefanywa ilihali wao wapo.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Wakuu wa Mikoa, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu Wakuu na viongozi wa Mkoa wa Dodoma.

 

Picha mbalimbali Mhe. Rais Dkt. J.P.Magufuli akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua ikulu ya chamwino

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimthibitisha Bw.  James Wilbert Kaji kuwa Kamishna  Generali wa Mamlaka ya  udhibiti  wa Dawa za kulevya  nchini  (DCEA),  kabla ya kuapishwa   Kamishina Jenerali James Kaji alikua akikaimu nafasi hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aki ongea baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali alio waapisha ikulu ya chamwino  leo.

Kutoka kushoto   Katibu  Tawala  wa mkoa  wa Simiyu ,Mariam  Perla  Mmbaga,  Mkuu wa mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Philemon Rugumiliza Sengati na CP, Thobias  Emir  Andengenye  mkuu wa mkoa  wa Kigoma  wakila kiapo cha maadili baada ya kuapishwa mapema leo.

Wakuu wa wilaya wateule  wakila kiapo cha maadili  baada ya kuapishwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli  mapema leo julai 06-2020

 Bi. Mariam  Perla  Mmbaga akiapa mbele ya  Mhe. Rais  Dkt. J.P.Magufuli  Kuwa Katibu  Tawala  wa mkoa  wa Simiyu  hafla iliofanyika  ikulu ya Chamwino  Dodoma   julai 06 – 2020

   Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha CP wa Polisi Thobias Emir Andengenye kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Dodoma Julai 6, 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia Mkuu wa Morogoro Mhe. Loatha Ole  Sanare akimuapisha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Ismail Twahir Mlawa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Dodoma Julai 6, 2020.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuliakishuhudia Mkuu wa Mkoa wa Pwani akimuapisha Mhandisi Martine Ntemo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Dodoma Julai 6, 2020

Wateuliwa wakila kiapo cha maadili ya Viongozi mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Dodoma Julai 6, 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na watumishi na viongozi mbalimbali  baada ya  hafla ya uapisho wa viongozi mbalimbali aliowateua  kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Dodoma Julai 6, 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiondoka baada ya kumalizika kwa hafla ya  kuwaapisha viongozi mbalimbali alio waapisha ikulu ya chamwino  julai 06-2020.