Daily Archives: October 24, 2020

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 24 Oktoba, 2020 amezindua safari za treni ya abiria kati ya Dar es Salaam Tanga na Arusha ambazo zilisimama zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Uzinduzi wa safari hizo umefanyika Jijini Arusha ambapo Mhe. Rais Magufuli amepokea treni ya abiria iliyotoka Jijini Dar es Salaam na kupita katika reli iliyokarabatiwa na wataalamu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Ukarabati wa reli hiyo umeanza Desemba 2019 na kukamilika Septemba 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 14 kwa kutumia wataalamu na vijana wa Tanzania, na tayari treni imeshasafirisha abiria 50,576 na zaidi ya tani 26,000 za mizigo.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bw. Masanja Kadogosa amesema kuanza kwa safari za treni kati ya Dar es Salaam, Tanga na Arusha kumepunguza gharama za usafiri ambapo nauli ya abiria kati ya Dar es Salaam na Arusha ni shilingi 16,000 ikilinganishwa na shilingi 35,000 inayotozwa kwa usafiri wa mabasi, ilihali usafirishaji wa mizigo kwa tani ni shilingi 68,000 ikilinganishwa na shilingi 110,000 kwa kutumia malori.
Bw. Kadogosa ameongeza kuwa pamoja kurejesha usafiri wa treni wa kati ya Dar es Salaam, Tanga na Arusha, TRC inaishukuru Serikali kwa kuiwezesha kukarabati mabehewa ya mizigo 600 ambapo mabehewa 333 yamekamilika, kuunda vichwa vya treni vipya 23, kununua vichwa vipya 11 na kwamba shirika hilo limetenga eneo Jijini Arusha kwa ajili ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuweka eneo la kuhifadhi makontena ili wananchi wapokee mizigo yao ya kutoka nje ya nchi moja kwa moja Arusha.
Pia ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) kati Dar es Salaam na Dodoma ambapo sehemu ya kwanza ya kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro ujenzi umefikia asilimia 90 na sehemu ya pili ya kuanzia Morogoro hadi Makutupora Dodoma ujenzi umefikia asilimia 45.3.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TRC kwa kazi nzuri iliyofanya kukarabati miundombinu ya reli, mabehewa na vichwa vya treni na ameeleza kuwa mafanikio hayo yamedhihirisha kuwa Watanzania wanaweza bila kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi ama kampuni za nje ya nchi kuendesha mashirika ya Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bw. Masanja Kadogosa na bodi ya TRC kwa usimamizi mzuri wa shirika hilo ambalo lilionekana kupoteza mwelekeo na sasa linakuwa kimbilio la Watanzania na tegemeo la kujenga uchumi wa nchi.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa reli, Serikali imedhamiria kuiimarisha TRC ambapo katika mwaka ujao imepanga kununua mabehewa mengine 800 ya mizigo, 37 ya abiria na vichwa 39 vya treni.
Ametoa wito kwa Watanzania kutoihujumu miundombinu ya reli na badala yake washirikiane na TRC na vyombo vya dola kuilinda isiibiwe ama kuharibiwa.
Sherehe za uzinduzi huo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Elias Kwandikwa, Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama na viongozi wa Mkoa wa Arusha wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Bw. Idd Hassan Kimanta.

TAARIFA KWA VYOMBO HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ikulu Ndogo, Karatu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya watu 15 vilivyosababishwa na ajali ya barabarani baada ya basi la abiria kupinduka katika mteremko wa Kumnyange uliopo katika Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera.
Ajali hiyo ambayo imetokea leo tarehe 24 Oktoba, 2020 pia imesababisha watu 18 kujeruhiwa.
Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brig. Jen Marco Gaguti na amemtaka kufikisha salamu za pole kwa familia za Marehemu, ndugu, jamaa na wote walioguswa na vifo hivyo, na amewaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka na kuungana na familia zao.
“Nimesikitishwa na vifo vya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, nawapa pole wafiwa wote na nawaomba wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi kigumu cha majozi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wa barabara hasa madereva wa magari kuzingatia sheria zote za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
Pia amevitaka vyombo vinavyosimamia usalama barabarani kuchukua hatua dhidi ya watumiaji barabara wanaokiuka sheria za barabarani