Daily Archives: December 8, 2020

RAIS MAGUFULI AFANYA UKAGUZI WA UJENZI WA IKULU YA CHAMWINO NA KUSHIRIKI IBADA YA KUUAGA MWILI WA ALIEKUA JAJI MSTAAFU WA MAHAKAMA YA RUFANI ,HARLOD NSEKELA VIWANJA VYA CHINANGALI DODOMA

RAIS MAGUFULI AFANYA UKAGUZI WA UJENZI WA IKULU YA CHAMWINO , DODOMA  

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 08 Desemba, 2020 amekagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Ikulu Mkoani Dodoma na kuelezea kuridhishwa na kiwango na kasi ya ujenzi wa majengo ya ofisi hizo unaofanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Ujenzi wa Ofisi hizo ulioanza tarehe 17 Februari, 2020 unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 3 ijayo na unafanywa kwa usanifu na muonekano sawa na Ofisi za Ikulu zilizopo Jijini Dar es Salaam.

Msimamizi wa ujenzi wa ofisi hizo, Luteni Kanali George William Nyisa amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa ujenzi huo utakamilika kwa wakati uliopangwa.

Akikagua majengo yanayojengwa, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na uimara wa nguzo na kuta zinazojengwa na amesema ni fahari kubwa kwa Taifa kujenga ofisi yake ya Ikulu kwa kutumia Jeshi badala ya kutumia wakandarasi kutoka nje ya nchi.

Mhe. Rais Magufuli pia amezungumza na Vijana wa JKT wanaoshiriki ujenzi huo ambapo amekumbusha ahadi yake kuwa vijana hao 2,424 wataandikishwa katika JWTZ mara watakapomaliza jukumu la ujenzi wa Ofisi za Ikulu.

Pamoja na kuwapongeza vijana hao, Mhe. Rais Magufuli pia amewapongeza vijana wa kiraia wanaoshiriki katika ujenzi huo ambao ni mafundi, na amewaahidi kuwa atawaangalia mara baada ya kumaliza kazi hiyo.

 

 

RAIS MAGUFULI ASHIRIKI IBADA YA KUUAGA MWILI WA ALIEKUA JAJI MSTAAFU WA MAHAKAMA YA RUFANI  ,HARLOD NSEKELA  VIWANJA VYA CHINANGALI DODOMA .

Mapema leo asubuhi, Mhe. Rais Magufuli amewaongoza wananchi wa Dodoma kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Harold Nsekela aliyekuwa Kamishna wa Maadili, ambaye amefariki dunia tarehe 06 Desemba, 2020 Jijini Dodoma.

Viongozi wengine waliotoa heshima za mwisho ni pamoja na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi.