Daily Archives: February 19, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 19 Februari, 2021 ameongoza viongozi na wananchi kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Balozi (Mhandisi) John William Hubert Kijazi katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam. 

Viongozi wengine waliotoa heshima za mwisho pamoja na Mhe. Rais Magufuli ni Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Naibu Spika Mhe. Tulia Ackson, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Bw. Aboubakar Kunenge.

Katika salamu zake Mhe. Rais Magufuli amemuelezea Marehemu Balozi Kijazi kuwa alikuwa kiongozi mahiri, muadilifu, mnyenyekevu, msikivu, mcha Mungu, asiyejikweza, asiyetaka makuu na mwenye huruma na upendo mkubwa kwa viongozi wenzake, watumishi na jamii kwa ujumla jambo lililomfanya kuwa kipenzi cha watu.

Mhe. Rais Magufuli amesema kutokana na uadilifu wake wa hali ya juu tangu akiwa Mhandisi wa Barabara wa Mkoa wa Dodoma na baadaye kuwa Mkurugenzi wa Barabara wa Wizara ya Ujenzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Balozi wa Tanzania nchini India aliamua kumteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kuanzia mwaka 2016 hadi mauti yalipomkuta tarehe 17 Februari, 2021 kazi ambayo ameifanya vizuri.

Mhe. Rais Magufuli ametoa pole kwa familia ya Marehemu Balozi Kijazi na amemuomba Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amerudia kutoa salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kufuatia kifo cha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki dunia tarehe 17 Februari, 2021 na kuzikwa jana tarehe 18 Februari, 2021 huko Pemba.

Mhe. Rais Magufuli amemuelezea Maalim Seif Sharif Hamad kuwa alikuwa kiongozi aliyependa amani na umoja licha kufanya siasa zake kupitia vyama vya upinzani pamoja na utayari wake wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani Zanzibar ambapo mpaka mauti yanamkuta alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Amefafanua kuwa hata alipokutana nae Jijini Dar es Salaam baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na alipokutana nae alipomtembelea nyumbani kwake Chato Mkoani Geita tarehe 14 Januari, 2021, Maalim Seif Sharif Hamad alisisitiza kuwa hatowahamasisha wafuasi wake kufanya vurugu na kuvunja amani na alipenda kuwepo umoja wa Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla. Hivyo amewataka Watanzania kumuenzi kwa kudumisha amani na umoja uliopo.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuondoa hofu katika kipindi hiki ambacho dunia inapita wakati mgumu wa kukabiliana na janga la ugonjwa wa Korona na badala yake wachukue tahadhari na kumtanguliza Mungu, na ametangaza siku 3 za maombi na kufunga ambapo Waislamu wameanza leo, Wasabato kesho na Wakristo wengine Jumapili.

Mhe. Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya kutishana na uzushi vinavyofanywa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo uzushi uliofanywa dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipando Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango aliyezushiwa kafariki dunia ilihali yupo hai na anaendelea vizuri na matibabu.

Amesisitiza kuwa Serikali haina mpango wa kufungia watu majumbani mwao (lockdown) na kwamba Mungu aliyeiepusha Tanzania na madhara makubwa ya ugonjwa wa Korona mwaka jana ataiepusha na mwaka huu.

Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akitoa heshima za mwisho wakati wa ibada ya kumuga Balozi John William Kijazi aliekua Katibu Mkuu Kiongozi ,Balozi Kijazi anatarajiwa kuzikwa leo 19 Februari 2021 kijijini kwake Korogwe mkoa wa Tanga.

PICHA; MHE.MAGUFULI ASHIRIKI IBADA YA KUAGA MWILI WA BALOZI JOHN WILLIAM KIJAZI ALIEKUA KATIBU MKUU KIONGOZI