Daily Archives: February 25, 2021

UFUNGUZI WA SOKO KISUTU NA JENGO LA CHAMA LA JITEGEMEE LUMUMBA.




Rais wa. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akizundua rasmi jengo la Jitegemee House pamoja na Studi za Channel Ten Plu,Radio Magic FM na Radio Classic FM leo Alhamisi Februari 25, 2021
Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli akifurahi bada ya kuutazama wimbo aliouomba wa mwanamziki Prof. Jay na Stamina uitwao Baba na kuangalia wimbo akiwa studio za AMG inayomiliki Channel Ten Channel Ten Plus radio classic na radio Magic FM
Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na mtangazaji Salum Mkambaya kabla ya kuomba kupigiwa wimbo wa mwanamziki Prof. Jay na Stamina uitwao Baba na kuangalia wimbo akiwa studio za AMG inayomiliki Channel Ten Channel Ten Plus radio classic na radio Magic FM

Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na mtangazaji Salum Mkambaya kabla ya kuomba kupigiwa wimbo wa mwanamziki Prof. Jay na Stamina uitwao Baba na kuangalia wimbo akiwa studio za AMG inayomiliki Channel Ten Channel Ten Plus radio classic na radio Magic FM

Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na wafanyakazi wa Kampuni ya habari ya chama , AMG inayomiliki Channel Ten Channel Ten Plus radio classic na radio Magic FM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akiagana na wananchi na viongozi wa Dar es salaam alipomaliza
kuwahutubia katika mkutano wa hadhara viwanja vya Mnazi Mmoja jijini
baada ya kuzindua Soko Kuu la Kisutu pamoja na Studio za Channel Ten.
Plus TV, Radio Magic FM. na Radio Classif FM leo Alhamisi Februari 25,
2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Soko Kuu la Kisutu
leo Alhamisi Februari 25,2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 25 Februari, 2021 ameendelea na ziara yake Mkoani Dar es Salaam ambapo ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Soko Kuu la Kisutu, amezindua jengo la Jitegemee na amezindua vyombo vya habari vya kampuni ya Afrika Media Group Limited inayomiliki vituo vya luninga vya Channel Ten na Channel Ten Plus, na vituo vya redio vya Magic FM na Classic FM.

Soko Kuu la Kisutu lenye ghorofa 4 kwenda juu na 1 kwenda chini (basement) limejengwa upya likiwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 1,500 ikilinganishwa na soko la zamani lililokuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 669, kuegesha magari 40, lina maeneo ya huduma za kijamii na lina eneo la ukubwa wa meta za mraba 11,935.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga amesema ujenzi wa soko hili ambao umefikia zaidi ya asilimia 95 utagharimu shilingi Bilioni 13.484 (fedha zote zikiwa zimetokana na makusanyo ya ndani ya iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala) na kukamilika kwake kutawahakikishia wazalishaji wa bidhaa hasa wakulima kupata soko na kuinua kipato cha wafanyabiashara wakiwemo wafanyabiashara wadogo (Machinga) takribani 2,000.

Jengo la Jitegemee ambalo linamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) limekarabatiwa kwa gharama ya shilingi Milioni 800 baada ya kutelekezwa kwa takribani miaka 16. 

Jengo hilo la kihistoria lilijengwa mwaka 1961 na Chama cha TANU ambacho kutokana na Wakoloni kutotaka kujenga vyuo vikuu kwa ajili ya Watanzania kiliamua majengo hayo yatumike kuanzisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Bashiru Ally Kakurwa amesema CCM inajisikia fahari kuwa chimbuko la kupigania elimu kwa Watanzania kwa kuanzisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (kikiwa na wanafunzi 14) ambacho leo kimekua hadi kuwa shule 7, ndaki 7, Vyuo Vikuu Vishiriki 2, Taasisi 6 na wanafunzi 35,330.

Baada ya kuzindua jengo hilo, Mhe. Rais Magufuli amezindua na kukagua vyombo vya habari vya kampuni ya Africa Media Group Limited inayomilikiwa na CCM ambavyo ni Channel Ten, Channel Ten Plus, Magic FM na Classic FM ambavyo pamoja na kuhamishiwa katika jengo hilo vimefungwa mitambo na vifaa vipya vya matangazo.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ambayo kutokana na kuongoza katika ukusanyaji wa mapato ya ndani hapa nchini imefanikiwa kujenga Soko Kuu la Kisutu kwa kutumia fedha zake, na amesema baada ya kuipandisha hadhi na kuwa Jiji la Dar es Salaam Meya na Naibu Meya waliokuwa wa Manispaa ya Ilala ndio watakuwa Meya na Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli ameeleza dhamira yake ya kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linaboreshwa kwa miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii na amebainisha kuwa Soko Kuu la Kisutu ni kati ya Masoko 22 yaliyojengwa katika miji mbalimbali hapa nchini kwa gharama ya shilingi Bilioni 119.921 na vituo vya mabasi 18 ambavyo vimewekewa ta ana kujengwa barabara za kuingia na kutoka.

Mhe. Rais Magufuli ametaka Soko Kuu la Kisutu litunzwe vizuri, amewataka wafanyabiashara kuwa waadilifu kwa kulipa kodi inavyostahili badala ya kukwepa kwa kutumia Wamachinga na ametaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujirekebisha kwa kutenda haki kwa wafanyabiashara kwani baadhi ya maafisa wake wamekuwa wakiwatisha wafanyabiashara kwa makadirio makubwa ya kodi ili kupata mwanya wa kupokea rushwa.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza CCM kwa uwekezaji mzuri wa jengo la Jitegemee na amewapongeza wafanyakazi wa Africa Media Group Limited wakiwemo waandishi wa habari na Watangazaji ambao amewataka kufanya kazi kwa weledi na kutanguliza maslahi ya Taifa.

Amewataka Waandishi wa Habari wote hapa nchini kujiepusha na uchochezi, uzushi, upotoshaji na kuichafua nchi na badala yake watoe ushirikiano kwa kuandika na kutangaza habari zinazojenga umoja, mshikamano na maendeleo huku akitoa wito kwa viongozi na maafisa wa Serikali kutoa taarifa pale vyombo vya habari vinapohitaji.

Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inajali uhuru wa vyombo vya habari na kuthibitisha hili hata idadi yake imeongezeka kati ya mwaka 2015 na sasa ambapo redio zimeongezeka kutoka 106 hadi 193, Luninga zimeongezeka kutoka 25 hadi 46, redio za mtandaoni 23 na televisheni 440 zimesajiliwa na magazeti na majarida 247 yamepatiwa leseni hali inayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa idadi kubwa ya vyombo vya habari Afrika na Duniani.

Kesho, Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Dar es Salaam ambapo ataweka jiwe la msingi la mradi wa kiwanda cha ushonaji wa sare za Askari Polisi na kuzindua majengo ya Chuo cha Polisi Kurasini.