HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, AKIZUNGUMZA NA WAZEE WA MKOA WA DAR ES SALAAM, TAREHE 22 DESEMBA, 2014

Shukrani

Mheshimiwa Makamu wa Rais;

Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM;

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam; Viongozi wa CCM Mkoa;

Viongozi Wenzangu; Viongozi wa Dini; Wazee Wangu;

Wananchi Wenzangu;

Nawashukuru sana wazee wangu wa Dar es Salaam, kwa kukubali mwaliko wangu na kuja kuzungumza nami siku ya leo. Natambua kuwa taarifa ilikuwa ya muda mfupi lakini mmeweza kuja kwa wingi kiasi hiki. Naomba radhi kwamba ilikuwa tukutane Ijumaa lakini kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu tukaahirisha mpaka leo. Asanteni sana kwa uvumilivu wenu. Kama mjuavyo, kila ninapoomba kukutana nanyi ninalo jambo au mambo muhimu kitaifa ambayo napenda kuzungumza nanyi, na, kwa kupitia kwenu taifa zima linapata habari. Leo nina mambo mawili.

Wazee Wangu;

Kwanza kabisa, nataka kurudia kuwashukuru Watanzania wenzangu kwa moyo wenu wa upendo mliouonyesha kwangu katika kipindi chote cha matibabu yangu nikiwa nje na hata baada ya kurejea nchini. Kwa kweli nina deni kubwa kwenu.  Lazima nikiri kuwa, salamu zenu na taarifa kwamba watu wamekuwa wananiombea uponaji wa haraka na uzima zinanipa faraja kubwa na kunitia moyo. Nadhani zimechangia sana kuifanya afya yangu kuendelea kuimarika kila kukicha. Bado sijawa “fit” kabisa lakini naendelea vizuri. Hali yangu ilivyo sasa sivyo ilivyokuwa wiki iliyopita au siku niliporejea nchini.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Ndugu Wananchi;

Jambo la kwanza ninalotaka kulizungumzia leo ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Jumapili iliyopita tarehe 14 Desemba, 2014 na jana tarehe 21 Desemba, 2014 katika maeneo ambayo uchaguzi huo uliahirishwa. Bila ya shaka sote tumesikia taarifa ya awali ya zoezi la upigaji kura iliyotolewa na Mheshimiwa Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tarehe 17 Desemba, 2014. Katika taarifa yake hiyo, Mheshimiwa Waziri alieleza kwamba kwa jumla zoezi limeenda vizuri kwenye maeneo mengi nchini. Uchaguzi ulifanyika kwa ukamilifu katika Halmashauri 141 kati ya 162. Katika Halmashauri 21 uchaguzi wake uliahirishwa na umefanyika jana tarehe 21 Desemba, 2014. Kwa jumla, katika maeneo mengi uchaguzi ulifanyika kwa salama na amani na hivyo kuwapa wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowapenda kuongoza vijiji vyao, vitongoji vyao na mitaa yao. Kufanyika kwa uchaguzi huu ni uthibitisho mwingine wa kuendelea kukomaa kwa demokrasia nchini. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa wale wote walioshiriki katika uchaguzi huu kwa maana ya vyama vya siasa na wagombea. Natoa pongezi maalum kwa walioshinda. Nawaomba sasa wakae chini kutengeneza mikakati na mipango ya kuwaongoza wananchi wa maeneo yao katika kupata ufumbuzi wa changamoto za maendeleo na za maisha, zinazowakabili.

Ndugu wananchi;

Katika taarifa yake hiyo pia, Waziri Hawa Ghasia alielezea masikitiko yake kuhusu kasoro za uendeshaji wa zoezi zilizojitokeza katika maeneo mbalimbali. Aidha, aliahidi kuchukua hatua stahiki za kinidhamu dhidi ya watendaji na viongozi wa Serikali waliosababisha kasoro hizo. Alifafanua kuwa miongoni mwa hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kufukuzwa kazi, kusimamishwa kazi, kushushwa cheo, kukatwa mshahara au kupewa onyo. Napenda kuelezea kufurahishwa kwangu na msimamo huo wa Waziri wa TAMISEMI na nampongeza kwa hatua alizochukua. Namuunga mkono na namtaka aendelee na msimamo huo katika kukabili vitendo vya utovu wa nidhamu wa watumishi wa umma. Lazima kila mtumishi wa umma ajue kuwa asipotimiza ipasavyo majukumu yake kuna adhabu inayolingana na kosa alilofanya. Isitoshe, watu hao ndio watakaoendesha na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwakani wakiwa mawakala na wasaidizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hivyo basi, kuwajibishwa wale waliozembea katika uchaguzi, itakuwa fundisho kwao na kwa wengine katika uchaguzi wa mwaka 2015 na chaguzi nyingine zijazo.

Ndugu wananchi;

Kwa upande wa ghasia, fujo na ugomvi uliotokea wakati wa zoezi la uchaguzi, nimezungumza na viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi na kuwataka kuhakikisha kuwa wale wote waliofanya vitendo vya kuvunja sheria wanatiwa nguvuni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Nimewataka wasifanye ajizi na watu wa aina hiyo. Hawa ni watu hatari ambao hawana budi kuchukuliwa hatua thabiti za kuwadhibiti na kuwaadabisha. Tusipofanya hivyo tunawakatisha tamaa raia wema na watiifu wa sheria. Aidha, watu wakikamatwa na kuachiliwa muda mfupi baadae, wakati mwingine hata bila dhamana ya namna yo yote inawachanganya sana watu wema. Isitoshe tutakuwa tunalea maradhi ya watu wabaya na kuwafanya waendelee kusumbua jamii. Nimewakumbusha kuwa wasipokuwa wakali sasa tunaweka mazingira ya hatari ya kuja kutokea mambo mabaya zaidi mwaka ujao kwenye uchaguzi mkuu.

Sakata la Akaunti ya Tegeta ESCROW Ndugu Wananchi;

Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia si geni masikioni kwenu, nalo ni sakata la Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti mwezi Juni, 2014, kulitolewa madai kuwa fedha zilizokuwemo katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyoko Benki Kuu zimechotwa kinyemela na mmiliki wa Kampuni ya Pan African Power Solution (PAP) akishirikiana na Maafisa wa Serikali. Serikali iliahidi kufanya mambo mawili. Kwanza, kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa Akaunti hiyo na kwamba taarifa yake itawasilishwa Bungeni. Na, pili, kumuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa mwenendo mzima wa miamala katika Akaunti hiyo na kama kuna uhalifu wo wote uliopo kwenye mamlaka yake achukue hatua zipasazo kwa mujibu wa mamlaka na madaraka aliyonayo.

Ndugu Wananchi;

Yote mawili tuliyoahidi tumefanya. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amefanya ukaguzi wa miamala katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyoko Benki Kuu na taarifa yake ilishawasilishwa Bungeni. Pia niliagiza taarifa hiyo ichapishwe kwenye magazeti na tovuti ya Serikali ili watu waweze kuisoma. Agizo hilo nalo limetekelezwa. TAKUKURU wameendelea na uchunguzi wao na watakapomaliza na kuridhika kuhusu makosa yaliyofanywa watawafikisha wahusika Mahakamani. Mkurugenzi Mkuu wa PCCB alifika kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali na kutoa baadhi ya mambo kuhusu suala hili aliyoyaona ni muhimu Kamati iyajue.

Mambo Manne Makuu Ndugu Wananchi;

Tarehe 8 Desemba, 2014 nilipoanza kazi baada ya mapumziko ya ugonjwa nilikabidhiwa taarifa mbalimbali kuhusu sakata hili. Tangu wakati huo nimekuwa nazisoma pamoja na kuzungumza na watu mbalimbali na kuagiza nipatiwe ufafanuzi wa mambo mbalimbali kutoka kwa wahusika. Shabaha yangu ni kuyaelewa vizuri mambo hayo ili niweze kufanya uamuzi ulio sahihi na wa uhakika. Nimebaini kuwa yapo mambo makuu manne:- (a) Akaunti ya ESCROW (b)Miliki ya PAP kwa IPTL (c)Kodi za Serikali, na (d)Tuhuma za Rushwa

Akaunti ya ESCROW Ndugu Wananchi;

Katika Mikataba ya Kununua Umeme (Power Purchase Agreements) ambayo TANESCO imetiliana sahihi na kampuni binafsi za kuzalisha umeme za IPTL, SONGAS, SYMBION POWER na AGGRECO, kuna malipo ya namna mbili yanayofanywa na TANESCO. Kwanza, hulipia umeme ilionunua kutoka kwa kampuni hizo yaani tozo ya umeme (energy charges). Na, pili hulipia gharama za uwekezaji uliofanywa na kampuni hizo, yaani tozo ya uwekezaji (capacity charges). Katika mikataba yote hiyo imekubaliwa kuwa iwapo kutatokea kutofautiana, au mzozo unaohusu uwekezaji, upo utaratibu wa usuluhishi. Utaratibu huo unataka kwanza kufanyike mazungumzo, wakishindwa kuelewana watafute mtu wa kuwashauri na kuwasuluhisha; wakishindwa kukubaliana wapeleke shauri lao kwenye Kituo (Mahakama) cha Kimataifa cha Usuluhisi wa Migogoro ya Uwekezaji, (International Centre for Settlement of Investment Disputes – ICSID) kilichopo London, Uingereza

Ndugu Wananchi;      

Mwaka 1998 TANESCO walifikisha kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji, London, malalamiko kwamba gharama za uwekezaji za IPTL ni kubwa mno kuliko kiasi halisi walichowekeza. Mwaka 2001 Kituo cha Usuluhisi kilifanya uamuzi wa shauri hilo. Madai ya TANESCO yalikubaliwa kuwa uwekezaji halisi uliofanyika ni Dola za Marekani 127 na siyo Dola milioni 163.17 walizodai IPTL. Kutokana na kupungua huko kwa gharama za uwekezaji, tozo ya uwekezaji (capacity charges) nayo ilipunguzwa kutoka Dola za Marekani milioni 3.6 kwa mwezi mpaka Dola za Marekani milioni 2.6 kwa mwezi. Kituo pia, kilitoa mwongozo kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo.

Ndugu Wananchi;

Miaka minne baadaye TANESCO ilianza vuguvugu la kutaka kupata nafuu zaidi. Waliamua kugomea kulipa tozo ya uwekezaji kwa mkokotoo wa mwaka 2001. Nimeambiwa kuwa wanasheria wa TANESCO walishauri Shirika hilo lidai ukokotoaji kiwango cha tozo ya uwekezaji wa IPTL ufanyike kwa kuzingatia thamani ya hisa walizolipia wawekezaji ambayo ni shilingi 50,000 badala ya kutumia msingi wa mtaji uliotokana na mkopo wa Dola za Marekani milioni 38.16 wa wanahisa uliotumiwa na usuluhisho wa kwanza ICSID-1. Wakati wakisubiri mchakato wa usuluhishi wa mzozo huu mpya kuanza, pande zote mbili zilikubaliana kuanzisha Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Tarehe 5 Julai, 2006, akaunti hiyo ikaanzishwa kwa mkataba uliyotiwa sahihi na IPTL upande mmoja na Wizara ya Nishati na Madini kwa niaba ya TANESCO upande mwingine. Aidha, Benki Kuu iliteuliwa kuwa wakala wa kutunza akaunti hiyo nayo ilitia sahihi.

Ndugu Wananchi;

Kwa mujibu wa mkataba huo, Kampuni ya IPTL iliendelea kupeleka madai ya tozo ya uwekezaji kwa TANESCO ambayo nayo iliwajibika kulipa madai hayo. Malipo hayo yalitakiwa kupelekwa kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta tofauti na ilivyokuwa kabla ambapo yalipelekwa IPTL moja kwa moja. Utaratibu huu mpya ulikubaliwa kutumika hadi pande mbili zitakapofikia mwafaka kuhusu kiwango cha ukokotoaji.   Kwa upande wa malipo ya gharama ya umeme (energy charges) TANESCO imeendelea kulipa moja kwa moja kwa IPTL bila kupitia Akaunti ya Tegeta ESCROW maana hizo hazikuwa na mgogoro.

Ndugu Wananchi;

Kwa miaka saba tangu tarehe 5 Julai, 2006, akaunti hiyo ilipoanzishwa mpaka tarehe 5 Septemba, 2013, wakati Mahakama Kuu ilipokabidhi shughuli zote za IPTL kwa PAP, hakuna hatua stahiki zilizochukuliwa kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa tozo ya uwekezaji baina ya ITPL na TANESCO. Pande mbili husika hazikuwahi kukaa kuzungumza na wala hakuna shauri lililofikishwa kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Mogogoro ya Uwekezaji kama ilivyofanyika mwaka 1998. Wakati wote huo, TANESCO iliendelea kulipa madai ya tozo ya uwekezaji ya IPTL na kupeleka malipo hayo kwenye Akaunti ya Escrow. Ulipaji ulisimama katika kipindi kifupi wakati kampuni ya IPTL ilipowekwa kwenye ufilisi. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, wakati akaunti hiyo inafungwa tarehe 20 Novemba, 2013, kulikuwa na fedha taslimu shilingi 8,020,522,330.37; Hatifungani zenye thamani ya shilingi 159,231,370,000 na Dola za Marekani 22,198,544. Fedha zote hizo ni sawa na shilingi bilioni 202.9.

Ndugu Wananchi;

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kama TANESCO ingelipa tozo ya uwekezaji ipasavyo, wakati huo Akaunti hii ingekuwa na shilingi bilioni 306.7. Kwa sababu ya kutolipa fedha zote ipasavyo, wakati Akaunti inafungwa TANESCO walikuwa wanadaiwa na IPTL shilingi bilioni 103.8.   Kwa mujibu wa Mkataba wa Mauzo ya Umeme (PPA) malipo yaliyocheleweshwa, yanatozwa riba ya asilimia mbili ya fedha zote ambazo hazikulipwa kwa wakati. Hivyo basi, riba iliyotokana na TANESCO kuchelewesha malipo ilikuwa Dola za Marekani milioni 33.6. Ni matumaini yangu kuwa ufafanuzi uliotolewa katika Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unasaidia kuweka kumbukumbu sawa na sahihi kuhusu kiasi gani kilichokuwepo kwenye Akaunti ya ESCROW siku uamuzi wa Mahakama ulipofanya akaunti hiyo ifungwe. Kwa kifupi Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaeleza kuwa Akaunti hiyo ilikuwa na shilingi bilioni 202.9 na siyo shilingi bilioni 306.7 kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Fedha za Nani Ndugu Wananchi;

Ni matumaini yangu pia kwamba maelezo haya kwa kiasi fulani yamesaidia kutoa jibu kwa swali maarufu la fedha za kwenye akaunti hii ni za nani? Je ni za umma au za IPTL? Pengine nianze kwa kuelezea Akaunti ya ESCROW ni nini? Akaunti ya ESCROW ni tofauti na akaunti nyingine tunazozijua katika Benki zetu ambazo mtu anaweka fedha zake. Kama tujuavyo, katika Benki zipo Akaunti za aina tatu ambazo wengi tunazifahamu na kuzitumia yaani Akaunti ya Akiba (Savings Account), Akaunti ya Hundi (Current Account) na Akaunti ya Muda Maalum (Fixed Deposit Account). Akaunti ya Escrow ni akaunti maalum inayoanzishwa kwa ajili ya kufanya kazi maalum, kwa masharti maalum na kazi hiyo ikiisha akaunti yenyewe hufungwa. Akaunti hiyo husimamiwa na wakala aliyeteuliwa kwa makubaliano ya wale wanaofungua akaunti hiyo. Wakala ndiye mwenye jukumu la kusimamia akaunti na kumlipa mwenye fedha wakati ukifika. Kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta pande mbili husika zilikubaliana kuwa Benki Kuu ndiyo iwe Wakala. Ni muhimu kujua kuwa akaunti hiyo ingeweza kufunguliwa kwenye Benki yoyote siyo lazima BoT. Akaunti ya Tegeta ESCROW ilifunguliwa BoT mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity charges) zilizokuwa zinalipwa na TANESCO kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa ambaye ni IPTL. Kabla ya hapo TANESCO ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa IPTL. Kama nilivyokwishasema, awali ilifanyika hivyo ili kutoa nafasi kwa pande hizo mbili husika kumaliza tofauti zao kuhusu kiwango cha tozo ya uwekezaji ya IPTL. Kimsingi basi, fedha hizi ni za IPTL kwani ndiye mlipwaji na ni malipo yanatokana na madai ya IPTL kwa TANESCO kuhusu tozo ya uwekezaji. Hata hivyo, kwa mujibu wa CAG, inawezekana katika fedha hizo kuna fedha za umma. Hi ni kwa namna mbili. Kwanza, kama mgogoro baina ya TANESCO na IPTL ungetatuliwa na kiwango cha tozo ya uwekezaji kupungua kama ilivyofanyika mwaka 2001 katika ICSID-1 na kama pande mbili husika zingekubaliana au kuagizwa kuwa punguzo hilo lianze kuhesabiwa tangu tarehe ilipofunguliwa Akaunti hiyo (tarehe 5 Julai, 2006), basi kungekuwepo pesa za kurejeshwa TANESCO. Maadamu hili halikufanyika mpaka Mahakama ilipofanya uamuzi uliosababisha akaunti hiyo kufungwa. Katika mazingira hayo fedha zote zinakuwa ni za IPTL maana hakuna madai ya TANESCO.

Ndugu Wananchi;

Namna ya pili ni ile ambapo katika fedha hizi kunaweza kuwepo fedha za umma na iwapo kuna kodi za Serikali ambazo hazijalipwa. Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuthibitishwa na TRA ni kwamba kulikuwa na kodi ya VAT ambayo haikulipwa. Nimeambiwa kuwa TANESCO ndiyo ilikuwa na wajibu wa kukata kodi hizo kabla ya kulipa madai ya IPTL lakini kwa baadhi ya malipo haikufanyika hivyo. Hivi IPTL inastahili kudaiwa kodi ya Serikali? Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa, kodi inayotakiwa kulipwa na IPTL ni shilingi bilioni 21.7. IPTL wameshapelekewa madai na TRA, na IPTL wamekubali kulipa. Katika ukaguzi wa Hesabu za TANESCO za mwaka 2012, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliwaelekeza TANESCO kuacha kuhesabu fedha zilizopo kwenye Akaunti ya ESCROW kama ni fedha zao. CAG aliwaambia TANESCO kwamba fedha hizo si zao.   Maagizo hayo ya CAG yanasomeka kama ifuatavyo: “As a result, the deposit balance in Escrow account does not meet the definition of an asset of the Company and therefore an adjustment has been made to de-recognize the asset and related liability to the tune of the amounts available in the Escrow account”   Kwa tafsiri yake ni kuwa: “Hivyo basi, fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya Escrow hazina sifa ya kutafsiriwa kama ni mali ya kampuni (TANESCO) hivyo, marekebisho yamefanywa ili kutotambua mali na madeni yanayohusu fedha hizo kwa kiasi cha fedha zilizopo kwenye akaunti ya Escrow.”   Kutokana na maelezo haya ni dhahiri kwamba, fedha zilizokuwa kwenye Escrow siyo za TANESCO na hazikupaswa kuingizwa kwenye vitabu vya TANESCO kama mali yake.

Chimbuko la Sakata Wazee Wangu;

Chimbuko la kadhia yote hii Bungeni na kwenye jamii ni uamuzi wa tarehe 5 Septemba, 2013, wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kuitambua PAP kuwa mmiliki halali wa IPTL na kuagiza Mfilisi akabidhi shughuli zote za IPTL kwa PAP. Katika utekelezaji wa uamuzi huo wa Mahakama Kuu ukazuka mjadala mkali kuhusu fedha zilizomo kwenye akaunti ya ESCROW kukabidhiwa kwa PAP. Kwanza kabisa mjadala ulikuwa ndani ya Serikali miongoni mwa viongozi na watendaji wa Wizara na Taasisi zinazohusika moja kwa moja na akaunti hiyo. Hizi ni Wizara ya Nishati na Madini, TANESCO na Benki Kuu. Viongozi na Watendaji husika walikuwa wanajiuliza na kuuliza kama walipe au wasilipe. Walipotaka ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakaelekezwa watekeleze uamuzi wa Mahakama Kuu. Alisema uko sawa na hauna matatizo. Halikadhalika, Benki Kuu walipoulizia kuhusu kodi za Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza kuwa hakuna kodi ya kulipwa. Kwa kuzingatia ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, malipo yakafanyika kwa IPTL tena bila ya kodi kulipwa. Baada ya malipo kufanywa ndipo mjadala huo ukahamia katika jamii na Bunge na kugeuka kuwa kadhia kubwa iliyochukua sura ya kashfa yenye dalili za rushwa na wizi.

Uamuzi Unaotiliwa Shaka Wazee Wangu na Ndugu Wananchi;

Kwa jumla uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu akaunti ya Escrow, ushauri wa Mwanasheria Mkuu kwa Serikali wa kuelekeza uamuzi huo utekelezwe na viongozi wa Serikali kutekeleza ushauri huo vimetiliwa shaka. Umeonekana kuwa haukuwa uamuzi sahihi na kwamba umeitia hasara nchi. Isitoshe uamuzi huo umeibua hisia za kuwepo harufu na vitendo vya rushwa. Wapo waliosema si bure iko namna! Wapo waliotaja majina na watu wanaodai wamepata mgao wa Escrow tena wengine wamechukua fedha kwa viroba, sandarusi na rumbesa. Bahati mbaya sana katika mjadala ilijengeka dhana isiyokuwa sahihi kwamba jambo hili lilianzishwa na Maafisa hao wa Serikali kwa nia ya kujinufaisha wao binafsi. Ukweli ni kwamba uamuzi ulifanywa na Mahakama Kuu na kwenye Serikali ilikuwa utekelezaji wa amri hiyo.

Wazee Wangu;

Nilipokutana na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata maoni yake kuhusu kadhia hii ameendelea kusema alichosema Bungeni kuwa hakukosea katika ushauri wake na wala Mahakama haikufanya makosa. Hivyo basi, hakuona sababu ya kwenda Mahakamani kuomba marekebisho ya uamuzi wa Mahakama kuhusu fedha zilizokuwepo kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta kukabidhiwa kampuni ya PAP mmiliki wa IPTL. Vilevile haoni kama kuna hasara yo yote ambayo nchi imepata kwa sababu fedha zile ni za IPTL na imelipwa IPTL. Akifafanua, alisema kuwa akaunti ya Escrow ilianzishwa kwa ajili ya kutunza fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji kwa IPTL yaliyokuwa yanafanywa na TANESCO. Kabla ya mzozo kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo na kuanzishwa kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta, TANESCO ilikuwa inalipa tozo ya uwekezaji moja kwa moja kwa IPTL. Baada ya kutokea mzozo na akaunti kuanzishwa mambo mawili hayakubadilika. Kwanza kwamba IPTL haikuacha kupeleka madai ya tozo ya uwekezaji kwa TANESCO. Na, pili, kwamba TANESCO haikuacha kulipa madai hayo. Mdai na mdaiwa hawakubadilika. Kuwepo kwa akaunti ya Escrow hakubadili mwenye fedha zake. Akaunti hiyo iliundwa kuhifadhi fedha za IPTL wakati suluhu inatafutwa kuhusu kiwango cha tozo. Matumaini ni kwamba kama kiwango kitapunguzwa, TANESCO inaweza kupata nafuu ya malipo. Kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu kuruhusu IPTL ilipwe fedha za akaunti ya Escrow, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema ni uamuzi sahihi na wala taifa halikupata hasara kwa sababu pesa zimelipwa IPTL na siyo mtu mwingine. Isitoshe anaona uamuzi wa Mahakama umeisaidia TANESCO kutua mzigo mkubwa iliyokuwa nao kwa miaka saba. Kama mjuavyo, akaunti ya Escrow ilianzishwa kuhifadhi pesa za malipo ya tozo ya uwekezaji ya IPTL. Ilianzishwa kwa matumaini kuwa TANESCO watapata nafuu ya tozo ya uwekezaji. Lakini, hapakuwahi kufanyika mazungumzo baina ya TANESCO na IPTL kuhusu jambo hilo na wala suala hilo halijafikishwa ICSID. Haikuweza kufanyika hivyo kwa sababu washauri wa kisheria wa TANESCO hawajafanya hivyo. Wapo wanaodai kuwa hawafanyi hivyo kwa sababu hakuna sababu mpya zinazoweza kupatikana kuifanya ICSID ibadili uamuzi wake wa 2001 kuhusu kiasi cha tozo na namna ya ukokotoaji wake. Matokeo yake ni TANESCO kuwa na akaunti ya Escrow ambayo mwisho wake haujulikani. TANESCO inaendelea kudaiwa na IPTL tozo ya uwekezaji na kulazimika kulipa kwenye akaunti hiyo. Kwa masharti ya akaunti ya Escrow wanaposhindwa kulipa wanatozwa riba. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG mpaka tarehe 20 Novemba, 2013, TANESCO ilikuwa inadaiwa shilingi bilioni 103.8 ambazo hawajalipa kwenye akaunti ya Escrow na riba ya Dola za Marekani milioni 33. Kwa sababu hiyo basi uamuzi wa kufunga Akaunti ya Tegeta Escrow unalipatia unafuu TANESCO dhidi ya kulimbikiza madeni na riba. Kwa upande wa kodi za Serikali ambazo hazikulipwa, Mheshimiwa Jaji Werema alisema yeye alitoa ushauri tu. Hata hivyo, kama mamlaka husika inaona zipo kodi zinazostahili kulipwa izidai. Hakuna kilichopotea kwa sababu anayedai, yaani TRA yupo, na mdaiwa yupo, IPTL. Uamuzi wa ICSID II Kuhusu Tozo ya Uwekezaji

Wazee Wangu;

Yalitolewa mawazo kuwa kama fedha za akaunti ya Tegeta Escrow zingelipwa baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Kusuluhisha Migogoro ya Uwekezaji (ICSID II) kutoa uamuzi wake, TANESCO ingepata nafuu ya kupungua kwa tozo ya uwekezaji. Kuhusu jambo hilo nimeambiwa kwamba kuna mambo mawili ya msingi. Kwanza kwamba Mahakama hiyo haikutoa viwango vipya vya tozo kama ilivyofanya mwaka 2001 kwenye ICSID–I.   Haikubadili mwongozo wa ukokotoaji wa tozo. Imesema madai yanaweza kuzungumzwa na kusisitiza kuwa katika mazungumzo hayo TANESCO watambue kwamba wanahisa waliwekeza mtaji wao binafsi wakati wa kununua mtambo na pia walikopa madeni, na kwamba kiasi cha fedha walichowekeza kilitakiwa kiwe na kiwango cha juu zaidi cha faida. Jambo la pili ni kwamba, shauri hili la pili la ICSIDI II halikuihusisha kampuni ya IPTL mwenye Mkataba wa Kuuza Umeme na TANESCO na siyo Benki ya Standard Charterd. IPTL wameweka pingamizi la utekelezaji wa uamuzi wa shauri hilo hapa nchini, hivyo inakuwa vigumu kwa TANESCO kufanya mazungumzo kwa msingi wa shauri hilo. Kinga Dhidi ya Madai Wakati wa kufunga akaunti ya Escrow, upande wa Serikali ulielezea hofu yake ya uwezekano wa siku za usoni mtu kudai tena kulipwa fedha hizi hizi ilizolipwa PAP. Nimeambiwa kuwa suala hilo haliwezi kutokea kwani limetengenezewa wigo imara wa kimkataba kuzuia.   PAP imetiliana sahihi na Serikali kwamba iwapo kutatokea mdai yo yote PAP itawajibika kulipa.

Mashaka ya Miliki ya PAP kwa IPTL Ndugu Wananchi;

Hofu nyingine kuhusu uwezekano wa Serikali kupata hasara ni yale madai kuwa huenda miliki ya PAP kwa asilimia 70 za hisa za IPTL zilizokuwa za kampuni ya Mechmar Berhard ya Malaysia siyo halali. Pale mwanzoni ilidaiwa kuwa kampuni ya Mechmar ilipouza hisa zake kwa kampuni ya Piper Link ya British Virgin Islands ilikuwa chini ya mchakato wa ufilisi kule Malaysia. Kama ingekuwa hivyo, kisheria mtu hawezi kuuza hisa zake akiwa kwenye mazingira hayo. Katika uchunguzi wa CAG alieleza kuwa amethibitisha kwamba madai hayo si kweli, Mechmar walipouza hisa zao tarehe 9 Septemba, 2010 kampuni haikuwa kwenye ufilisi. Iliingia kwenye mchakato wa ufilisi mwaka 2012. Lakini kwa upande wa kampuni ya Piper Link ya Uingereza inasemekana iliuza hisa hizo baada ya kuwa wamepokea amri ya Mahakama ya Malkia ya BVI kuizuia isiuze hisa hizo. Je ni kweli? Imefanyika hivyo? Kama ni kweli je PAP waliponunua hisa hizo walijua kama kuna zuio au hapana? Kama walijua basi na wao ni sehemu ya njama za kufanya udanganyifu. Kama hawakuwa wamejua basi wametapeliwa. Nimeagiza uchunguzi wa kina ufanyike kupata ukweli. Natambua hivi sasa Mahakamani zipo kesi zinazohoji uhalali wa PAP kumiliki asilimia 70 za hisa za Mechmar Berhad. Uchunguzi wetu hautaingilia mchakato huo lakini unaipa Serikali fursa nzuri ya kuchukua hatua zipasazo kuhusu suala hili lenye mjadala mkubwa.        Jambo lingine muhimu ambalo limeleta matatizo kwa Mahakama zetu nchini na BRELA ni uuzaji wa hisa za IPTL au kuwekwa rehani hisa hizo bila ya uamuzi huo kusajiliwa BRELA na kwenye Mahakama zetu. Sheria zetu ambazo ndizo za nchi ya Jumuiya ya Madola kama ilivyo kwa Hong Kong, Malaysia, na BVI, inaitaka kampuni ya Piper Link ya BVI iliponunua hisa za Mechmar katika IPTL kusajili BRELA ununuzi huo. Hali kadhalika, inaitaka SCB ya Hong Kong na kupata amri ya Mahakama kuzuia deni la Mechmar na kuwekwa dhamana ya hisa za Mechmar katika IPTL. Piper Link isiuze hisa 70 za Mechmar katika IPTL. Walitakiwa wasajili na BRELA na Mahakama yetu. Kutokufanya hivyo ndiko kunazua maneno mengi na mzozo kuhusu uuzaji wa hisa hizo kwa PAP. Kwa SCB wanapata usumbufu wa kudai madeni yao IPTL kwa sababu hiyo hiyo. Uchunguzi utakaofanyika utapata ukweli wa yote kwa uhakika.

Ndugu Wananchi;

Taarifa niliyopewa wakati najiandaa kuzungumza nanyi ni kuwa katika Mahakama zetu nchini kuna mashauri yahusuyo miliki ya PAP ya hisa 70 zilizokuwa za Mechmar katika IPTL na yapo mashauri yahusuyo PAP kupewa fedha za akaunti ya Escrow. Zipo pia nyingine za masuala mbalimbali yakiwemo mashauri yaliyofunguliwa na PAP dhidi ya watu, na makampuni binafsi na vyombo vya Serikali. Naamini uamuzi wa Mahakama zetu utatoa majibu kwa masuala yote hayo. Pamoja na hayo yatakayokuwa yanaendelea Mahakamani, Serikali itaendelea kufanya uchunguzi wake na kuamua namna ya kushughulikia taarifa zitakazopatikana ili nayo iweze kwenda Mahakamani itakapolazimu kufanya hivyo. Jambo lingine muhimu nataka uchunguzi wa kina ufanyike ni kujua nani ni nani katika uuzaji na ununuzi wa hisa za Mechmar. Hususan nataka tujue kwa ukweli na uhakika hisa hizo zimeuzwa kwa bei gani. Je, ni kweli gharama zinazosemwa ndizo zenyewe? Nataka kuthibitisha ukweli huo ili tujue kodi yetu ya ongezeko la mtaji (Capital Gains Tax) inayostahili kulipwa Tanzania ni kiasi gani? Je kiasi gani kimelipwa na kipi hakijalipwa ili kidaiwe?

Tuhuma za Kuwepo kwa Harufu ya Rushwa Wazee Wangu;

Kumekuwepo na tuhuma za vitendo vya rushwa katika mchakato mzima wa kufunga akaunti ya Escrow na kukabidhi fedha hizo kwa kampuni ya PAP. Halikadhalika, kumekuwepo na hisia hizo hizo kwa upande wa jinsi kampuni ya VIP Engineering and Marketing ilivyotumia pesa zake zilizoko kwenye Benki ya Mkombozi. Yamesemwa mengi sana na mmeyasikia na kuyasoma. Rushwa ni kosa la kijinai ambalo kwa Serikali yetu ni kosa ambalo ni vigumu kulivumilia wala kulifumbia macho.  Mara baada ya kupata fununu za uwezekano wa vitendo hivyo kufuatia taarifa ya awali ya CAG ya kwenda kukagua miamala, niliagiza taarifa husika zifikishwe kwenye Taasisi ya Kupamba na Kuzuia Rushwa (PCCB) kwa uchunguzi zaidi. Naambiwa taarifa hizo zimefika na kazi ya uchunguzi inaendelea. Tayari watu kadhaa wamehojiwa na wengine wanaendelea kuhojiwa. Wakati nawasihi wananchi kuvuta subira ili tuwape nafasi PCCB wakamilishe kwa ufanisi wa hali ya juu kazi yao waliyokwishaianza, nawaomba PCCB waongeze kasi ya uchunguzi. Napenda kufafanua kwamba kwa upande wa miamala iliyotoka katika akaunti ya kampuni ya VIP Engineering and Marketing ya Ndugu James Rugemalila, Serikali inashughulika na watumishi wa umma kwa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma, maana suala lao ni la kimaadili. Hatuwahoji wasiokuwa watumishi wa umma.

Maazimio ya Bunge Ndugu Viongozi;

Wazee Wangu; Ndugu Wananchi;

Niliona nianze kwa kutoa maelezo hayo ya utangulizi kabla ya kuyazungumzia maazimio ya Bunge. Serikali imepokea maazimio hayo ya Bunge na kuyafanyia kazi kwa ajili ya utekelezaji wake. Nawapongeza Wabunge wetu kwa moyo waliouonesha wa kuchukia maovu na kutaka yashughulikiwe ipasavyo. Napenda kuwahakikishia kuwa niko pamoja nao. Nampongeza Mheshimiwa Anna Makinda, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika na Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Mussa Zungu kwa uongozi wao mahiri. Hakika haikuwa kazi rahisi, lakini chini ya uongozi wao mambo yameisha salama na tumepata maazimio nane yanayozungumzika na kutekelezeka. Nawashukuru na kuwapongeza sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya uongozi wa Mheshimiwa Zitto Kabwe na Mheshimiwa Deo Filikunjombe na pia Wajumbe waliounda Kamati ya Mapendekezo kwa kufikia mwafaka wa mapendekezo haya 8 ambayo yaliazimiwa na Bunge. Mwisho lakini si ya mwisho kwa umuhimu, nawapongeza Wabunge wote kwa michango yao mizuri. Jambo lililonifurahisha sana ni ushirikiano wa Wabunge wa kambi zote katika kutafuta ufumbuzi wa suala hili muhimu,. Hivi ndivyo inavyotakiwa Bunge liwe. Kwa kweli lazima nieleze mshangao wangu niliposikia kambi ya upinzani ikijaribu kufanya maamuzi yale ni yao wao na wenzao hawamo. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ina Wajumbe 19 wa CCM na wa Upinzani 5. Bunge lina Wabunge wa CCM asilimia 74 na wa upinzani asilimia 26. Hivi kama ni yao wao pekee na wa upande wa CCM wangepinga yangekuwa? Yasingefika po pote, yangefia kwenye Kamati. Huku ni kutafuta umaarufu kwa mgongo wa wengine. Na, Wabunge wengi wa CCM na nyie semeni msikike kwa uamuzi mliyofanya wote. Napenda kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini hatuna upungufu wa dhamira ya kutekeleza yale maazimio yanayoangukia katika dhamana yetu. Napenda kuainisha mtazamo na mwelekeo wa Serikali katika utekelezaji wa maazimio hayo manane kama ifuatavyo:-  

Azimio la kwanza: Serikali iangalie uwezekano wa kuchukua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa mujibu wa Sheria za nchi.

Pendekezo tumelipokea, ni jambo linalowezekana kufanya. Hata hivyo, tunapopima ujumbe tunaoupeleka kwa jumuiya ya wawekezaji tunachelea kuwa inaweza kuleta hofu na kuwatisha wawekezaji waliopo na wajao. Nalisema hivyo kwa sababu sisi tuna historia ya kutaifisha mali za kamapuni binafsi. Hofu hiyo bado ipo. Tukichukua mitambo hii tunaweza kurudisha hofu za kurudi tulikokuwa na kukimbiza mitaji tunayohitaji kwa uchumi kukua na nchi kupata maendeleo. Nashauri tuendelee kuyapatia ufumbuzi matatizo ya IPTL kila tunapoyabaini. Aidha, Mahakama imetusaidia sana kwa kuamuru mitambo ya IPTL ibadilishwe ili itumie gesi asilia na kutoza bei ya umeme isiyozidi senti nane za Marekani. Tuyafuatiliye haya kwanza.  

Azimio la Pili: Azimio hilo linazungumzia kuhusu uwazi wa Mikataba linasomeka ifuatavyo: “Bunge limeazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti. Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme”.

Azimio hili tumelipokea na tunaangalia namna bora ya kulitekeleza ili kuweza kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza, kuitikia kilio cha muda mrefu kuhusu uwazi katika mikataba ambayo Serikali inaingia na wawekezaji; na pili kuhakikisha usiri wa mikataba hiyo ambayo ni haki ya wawekezaji hao dhidi ya washindani wao inazingatiwa. Serikali na Bunge tutakaa chini hivi punde kutafuta namna bora ya kisheria na tutafanya hivyo kwa kujifunza pia kutokana na uzoefu wa nchi ambazo zina utaratibu wa aina hii.  

Azimio la Tatu: Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba TAKUKURU, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama vichukue hatua stahili kwa mujibu wa sheria za nchi yetu dhidi ya watu waliotajwa kwenye taarifa maalum ya Kamati husika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya ESCROW, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusu kuhusika kwao katika vitendo hivyo vya jinai”

Vyombo husika vimekwishaagizwa kufanya hivyo na kazi imeanza na inaendelea. Ikiwa wapo watu wenye makosa hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.  

Azimio la nne: Linasomeka, “Kamati za Bunge kuwavua nyadhifa zao wenyeviti wa Kamati za Bunge waliotajwa kupewa fedha na kampuni ya VIP Engineering kabla ya kikao kijacho cha Bunge”

Azimio hilo liko chini ya mamlaka ya Bunge lenyewe. Nawaachia wao waamue.  

Azimio la Tano: Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania”

Azimio hili nimelipokea, tumelijadili hata hivyo, itabidi tufuate utaratibu wa kikatiba na kisheria wa kushughulikia masuala ya namna hiyo. Inatakiwa suala kama hili lianzie kwenye Mhimili wa Mahakama yenyewe na siyo kwa Rais au Bunge. Tume ya Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kumtaka Rais aunde Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua Jaji yeyote pale inaporidhika kuwa amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo. Nashauri suala hili tumuachie Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie atakavyoona inafaa.  

Azimio la Sita: “Bunge linaazimia kwamba mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Ltd. na benki yeyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka ya uchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya ESCROW kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (Institutions of money laundering concerns).

Pendekezo la Bunge ni zuri kwamba mamlaka husika na udhibiti wa vitendo vya utakatishaji fedha vifanye uchunguzi kwa mujibu wa Sheria. Serikali imelipokea na mamlaka husika yaani Financial Intelligence Units kulishughulikia. Naamini wameshaaza, tuwape muda watimize wajibu wao kwa mujibu wa sheria.  

Azimio la Saba: “Bunge liliazimia kwamba Serikali iandae, na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda TAKUKURU kwa lengo la kuanzishwa Taasisi mahsusi itakayoshughulikia kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Kazi ya kufanya mageuzi katika TAKUKURU inaendelea. Tayari Sheria mbalimbali zimetungwa ikiwa ni pamoja na Sheria Mpya ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2008, Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Fedha Haramu ya mwaka 1991 ambazo zote zinaweka utaratibu wa kushughulikia vitendo vya rushwa. Tutaendelea kuziboresha sheria hizo kwa kadri itakavyohitajika. Kazi iliyopo mbele yetu ni kuimarisha usimamizi wa sheria hizo. Jambo hilo nalo litazingatiwa katika maboresho hayo. Ni dhamira yangu na ya Serikali ninayoiongoza kupambana na kushinda vita dhidi ya rushwa. Kwa hiyo tuko tayari kulifanyia kazi pendekezo lolote linaloimarisha dhamira yetu hii njema.  

Azimio la nane: “Bunge linaazimia kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi na Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.

Azimio hili ndilo Azimio ambalo limevuta hisia za watu wengi, na pengine ndilo ambalo utekelezaji wake unasubiriwa kwa hamu. Utekeelzaji wake umeanza. Kwanza, ni kuhusu Bodi ya TANESCO,   tumeanza mchakato wa kuunda Bodi mpya kwani iliyopo imemaliza muda wake. Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni mtumishi wa umma anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa umma, hivyo nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameshajiuzulu. Tumelitafakari suala la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi la kupokea fedha kutoka VIP Engineering and Marketing ambazo kwa maelezo yake ni kwa ajili ya shule anayoimiliki na kuiendesha. Mwenyewe ameeleza wazi kupitia vyombo vya habari. Pamoja na hayo yapo mambo ya msingi kimaadili ambayo hayakuzingatiwa, hivyo tumemwomba atupishe tuteue mwingine. Kuhusu Prof. Muhongo nimemuweka kiporo, kuna uchunguzi niliagiza ufanywe na vyombo vyetu bado nasubiri taarifa hiyo ili nifanye uamuzi ndani ya siku chache zijazo.  

Hitimisho Wazee Wangu;   

Nawashukuruni kwa kunisikiliza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *