TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 05 Juni, 2020 amefungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na kuwahakikishia Walimu wote nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inathamini kazi kubwa wanayoifanya na itaendelea kuboresha maslahi yao na mazingira yao ya kazi.

Ufunguzi wa mkutano huo umefanyika katika uwanja wa CCM Jamhuri Jijini Dodoma na umehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa pamoja na viongozi na wanachama wa CWT 1,138 waliowakilisha mikoa 26 na wilaya 151 hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Rais wa CWT Mwl. Leah Ulaya na viongozi wenzake kwa kumkaribisha kufungua mkutano huo na amebainisha kuwa yeye pamoja na viongozi wengine wakiwemo Waziri Mkuu na Spika, hawakusita kukubali mwaliko huo kutokana na uongozi wa sasa wa CWT kujenga uhusiano mzuri na Serikali hali iliyowezesha kujenga daraja zuri la kushauriana na kushughulikia masuala mbalimbali yanayowahusu Walimu.

Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kuwepo uhusiano huo mzuri, Serikali imechukua hatua madhubuti za kuimarisha na kuboresha elimu zikiwemo kutoa elimu bila malipo ambapo kati ya Desemba 2015 na Februari 2020 imetoa shilingi Trilioni 1.01 kugharamia mpango huo, kuongeza shule za msingi kutoka 16,899 hadi kufikia 17,804, kuongeza shule za sekondari kutoka 4,708 hadi 5,330, kukarabati shule kongwe 73 kati ya 89 zilizopo, kujenga mabweni 253 na vyumba vya maabara 227, kutoa vifaa kwa maabara 2,956 pamoja na kuongeza madawati kutoka 3,024,311 hadi 8,095,207.

Juhudi zingine ni kukarabati vyuo vya walimu 18 na kujenga vyuo vipya 2, kupeleka kompyuta 1,550 katika vyuo 35 kwa lengo la kuimarisha ufundishaji wa masomo ya TEHAMA, kuongeza Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) kutoka 672 hadi 712, kukarabati na kuongeza vifaa katika vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) na kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kutoka shilingi Bilioni 341 hadi kufikia shilingi Bilioni 450.

Mhe. Rais Magufuli amesema juhudi hizo zimezaa matunda yenye manufaa makubwa kwa Watanzania kwani idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kuanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka Milioni 1 hadi Milioni 1.6 hivi sasa, idadi ya wanafunzi wa kidato cha 1 hadi cha 4 imeongezeka kutoka 1,648,359 hadi kufikia 2,185,037 na ufaulu wa wanafunzi umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Kuhusu maslahi ya Walimu, Mhe. Rais Magufuli amesema katika mwaka 2014/15 Watumishi wa Umma 306,917 walipandishwa vyeo ambapo kati yake 160,367 ni Walimu na kwamba katika mwaka huu Serikali itawapandisha vyeo Watumishi wa Umma 290,625 ambapo kati yake 166,548 ni Walimu.

Kuhusu malimbikizo ya madeni, Mhe. Rais Magufuli amesema tangu Novemba 2015 Serikali imelipa malimbikizo ya mishahara ya jumla ya shilingi Bilioni 115.3 ambapo kati yake shilingi Bilioni 38.3 wamelipwa Walimu wapatao 35,805. Serikali pia imelipa madeni yasiyo ya mishahara (likizo na uhamisho) ya shilingi Bilioni 358.1 na kwamba itaendelea kulipa madeni hayo kadiri uhakiki unavyofanyika.

Mhe. Rais Magufuli amezungumzia malipo ya mafao ya Walimu ambapo amesema kati ya Agosti 2018 na Juni 2020, Walimu 15,029 wamelipwa kiasi cha shilingi Trilioni 1.2 kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF na kwamba Walimu 2,631 waliobaki ambao wanadai shilingi Bilioni 215, watakuwa wamelipwa ifikapo Agosti 2020.

Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatambua kuwa kati ya Watumishi wa Umma wote 524,295, Watumishi 266,905 ni Walimu (sawa na asilimi 51) na kwamba pamoja na kuwaajiri walimu 22,342 katika kipindi hiki cha miaka mitano walimu wengine 13,526 wataajiriwa katika mwaka huu wa fedha.

Amewataka viongozi wa CWT watakaochaguliwa leo kuendeleza uhusiano mzuri na Serikali na kufanya kazi kwa kutanguliza maslahi ya Walimu badala ya maslahi yao wenyewe, pamoja na kusimamia vizuri mali na miradi ya chama hicho.

Rais wa CWT Mwl. Leah Ulaya na Katibu Mkuu wake Mw. Deus Seif wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ambao CWT inaupata kutoka Serikalini ikiwa ni pamoja na kuwapandisha vyeo Walimu, kutopunguza mishahara yao baada ya shule kufungwa kutokana na ugonjwa wa Corona, kulipa madeni ya Walimu na kuboresha mazingira ya kazi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *