TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

                               TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewasili Jijini Dar es Salaam akitokea Makao Makuu Dodoma.

Akiwa Ubungo, Mhe. Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma na kuelezea kufurahishwa kwake na kazi nzuri inayoendelea, pia amewasalimu wananchi wakiwemo viongozi na wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kando ya eneo la mradi huo.

Akizungumza kwa niaba viongozi wa vyama vya siasa na vijana wa Ubungo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Ubungo Ndg. Edwin Cyprian Mbena amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutekeleza vizuri na kwa vitendo Ilani ya CCM ikiwemo ujenzi wa barabara za juu katika eneo hilo, na ameeleza kuwa mradi huo umeleta heshima na unawanufaisha wananchi wa Ubungo na Jiji zima la Dar es Salaam.

Amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwaamini vijana na kuwapa nafasi za uongozi na amemuahidi kuwa vijana wamekubaliana kutomuangusha kwa kuhakikisha wanachapakazi na kusimamia maslahi mapana ya Taifa bila kubagua.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Ubungo kwa kupata mradi huo na ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatumia zaidi ya shilingi Bilioni 240 kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo na pia inajenga barabara ya njia nane (Kimara – Kibaha) kwa kuwa imedhamiria kuibadilisha Tanzania. Amewataka Watanzania wote kuunga mkono juhudi hizo.

Baada ya kuwasalimu wananchi hao, Mhe. Rais Magufuli ameendesha harambee ya kuchangia ununuzi wa pikipiki ya miguu mitatu kwa ajili Bi. Nyangoma James ambaye ni mwenye ulemavu, na amefanikiwa kukusanya shilingi 8,750,000/- zikiwemo shilingi 5,000,000/- alizotoa yeye mwenyewe.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *