Taarifa kwa vyombo vya Habari

 

Simu: 255-262961500/1
Nukushi: 255-262961502

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Julai, 2020 amewaongoza Watanzania kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa aliyefariki dunia tarehe 23 Julai, 2020.
Mwili wa Hayati Benjamin William Mkapa ulianza kuagwa tarehe 26 Julai, 2020 katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na kuhitimishwa leo ambapo pamoja na Mhe. Rais Magufuli na familia ya Hayati Mkapa, viongozi wengine wakiwepo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Jen. Alain Guillaume Bunyoni (kwa niaba ya Rais wa Burundi Mhe. Jen. Evariste Ndayishimiye) na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd wamepata fursa ya kutoa heshima za mwisho.
Wengine ni Waheshimiwa Maspika, Majaji Wakuu, Marais Wastaafu, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa na viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli amesema Taifa limepoteza mtu aliyetoa mchango mkubwa katika kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi, kuimarisha huduma za kijamii (elimu, maji, afya), kuanzisha na kuimarisha taasisi muhimu za Serikali, kuimarisha sekta binafsi, kujenga miundombinu hasa barabara na madaraja, kuinua ukusanyaji wa kodi, kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kimataifa, ukombozi na utatuzi wa migogoro ya Mataifa mbalimbali ya Afrika na aliyekuwa mahiri katika kuibua vipaji vya viongozi akiwemo yeye mwenyewe, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein na Mgombea wa Kiti cha Urais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa Hayati Benjamin William Mkapa ameacha mengi mazuri ya kujivunia na kuendelea kujifunza yakiwemo uongozi bora uliosimamia umoja, mshikamano, uchapakazi, uzalendo, uwajibikaji, uwazi na uhusiano mzuri wa kimataifa na ameahidi kuwa Serikali anayoiongoza itafanya kila liwezekanalo ili kudumisha na kuendeleza mambo yote mazuri yaliyoasisiwa nae.
Mhe. Rais Magufuli amesema yeye binafsi amefanyiwa mengi mazuri na Hayati Benjamin William Mkapa ambaye hakutaka aanguke kwa kumlea kama mwanae na kwa upendo mkubwa.
“Mzee Mkapa ni shujaa wangu na ni mtu muhimu sana katika historia ya maisha yangu, hata nilipopatwa na shida ama kukumbwa na changamoto mbalimbali, Mzee Mkapa hakuniacha, hivyo kuondoka kwake ni pigo kubwa sana kwangu kwa vile nimempoteza mtu muhimu sana katika maisha yangu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapa pole wanafamilia wakiongozwa na Mjane wa Hayati Benjamin William Mkapa, Mama Anna Mkapa na Watoto wake, amewaombea moyo subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na mpendwa wao.
Amewashukuru Watanzania wote kwa utulivu na mshikamano katika kipindi hiki cha maombolezo ya tangu Mhe. Benjamin William Mkapa afariki dunia, pia amewashukuru viongozi wa dini, vyombo vya ulinzi na usalama, vyombo vya habari, wageni mbalimbali na wote waliotuma salamu za rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa uliolikumba Taifa.
Mwili wa Hayati Benjamin William Mkapa umesafirishwa kwa ndege ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwenda kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara ambapo hapo kesho utazikwa kwa taratibu kidini na kwa heshima zote za kijeshi.

    

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *