Mhe . Rais Dkt. J. P. Magufuli aongoza Taifa kwenye maziko ya Hayati Benjamin W. Mkapa Rais wa awamu ya tatu maziko yalifanyika kijijini kwake Lupaso.

                                  TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Julai, 2020 amewaongoza Watanzania katika mazishi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa aliyezikwa kijijini kwake Lupaso, Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara.

Mazishi ya Mhe. Benjamin William Mkapa yamefanyika kwa taratibu za kidini na heshima zote za kijeshi ambapo Ibada ya Mazishi imeongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga (Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limefanya gwaride la mazishi likiambatana na kupiga mizinga 21 kwa heshima ya Rais Mstaafu na Amiri Jeshi Mkuu wa Awamu ya Tatu.

Viongozi mbalimbali wamehudhuria mazishi hayo wakiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

Viongozi wengine ni Maspika, Majaji Wakuu, Makamu wa Rais Wastaafu, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Maspika Wastaafu, Majaji Wakuu Wastaafu, Mawaziri na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi.

Pamoja na kuongoza Ibada ya mazishi, Askofu Mkuu Nyaisonga amesoma salamu za rambirambi za Baba Mtakatifu (Papa Francis) aliyewapa pole Watanzania wote na kuwataka kuwa wavumilivu na wenye matumaini na salamu za Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi na Rais Mstaafu wa Nchi hiyo Mhe. Joaquim Chissano zimesomwa na Balozi wa Msumbiji hapa nchini Mhe. Mónica Patrício Clemente.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein amesema wananchi wa Zanzibar wanaungana na Watanzania wenzao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na kiongozi shupavu na hodari aliyetoa mchango mkubwa kwa Taifa na katika kuuhifadhi na kuutunza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kwamba Wazanzibar daima watamkumbuka na kuuenzi mchango huo.

Marais Wastaafu Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wamemuelezea Hayati Benjamin William Mkapa kuwa alikuwa kiongozi hodari, mbunifu, aliyechukia umasikini na aliyeelekeza nguvu zake kujenga uchumi.

Wamempa pole Mhe. Rais Magufuli na familia ya Hayati Benjamin William Mkapa ikiongozwa na Mjane wake Mama Anna Mkapa kwa kuguswa zaidi na msiba huu mkubwa na wamewataka Watanzania wote waendelee kumuombea.

Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Watanzania kwa uvumilivu wao katika kipindi chote cha maombolezo, ameishukuru kamati ya maombolezo iliyoongozwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na amewashukuru viongozi wote wa Dini ambao walimlea tangu alipobatizwa na hata alipofariki dunia wamemuombea na kufanyia Ibada ya maziko.

Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kujifunza kutoka kwa Hayati Benjamin William Mkapa aliyewapenda Watanzania kwa dhati na aliyewapenda wanakijiji wenzake wa Lupaso kwani wakati wa uhai wake alipoulizwa azikwe wapi atakapofariki dunia alisema anataka azikwe kijiji cha Lupaso na sio Dodoma ambako kulikuwa na mapendekezo ya viongozi wakuu wa kitaifa kuzikwa makao makuu ya nchi.

Amewataka Watanzania wote waendelee kumuombea Hayati Benjamin William Mkapa apumzike kwa amani, na wamuombee Mama Mkapa na familia nzima ili waendelee kuwa wavumilivu na wastahimilivu baada ya kuondokewa na mpendwa wao.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa alifariki dunia tarehe 23 Julai, 2020 majira ya saa 3:30 usiku baada ya moyo wake kusimama ghafla (Cardiac Arrest) akiwa hospitali Jijini Dar es Salaam.

PICHA MBALIMBALI ZA MAZISHI YA RAIS MSTAAFU HAYATI B.W. MKAPA KIJIJINI  KWAKE LUPASO MASASI  MKOANI MTWARA  TAREHE 29 JULAI 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na mjane wa  Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa Lupaso Masasi mkoani Mtwara. wakati wa mazishi yake .

Mhe . Makamu wa Rais  Mama  Samia Suluhu Hassan  akibubujikwa na machozi wakati  mwili wa mazishi ya  Rais mstaafu wa Awamu Tatu  Benjamin W. Mkapa .

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mjane wa hayati Benjamini William Mkapa  Ana Mkapa  wakati wa Mazishi  ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa Kijijini  Lupaso Masasi mkoani Mtwara.

Katibu mkuu ofisi ya Rais  Utumishi  Dr. Laurian Ndumbaro akisoma  wasifu wa Marehemu Rais wa awamu Tatu Benjamini  William Mkapa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Viongozi mbalimbali pamoja Wananchi wa Lupaso waliohudhuria katika Mazishi  ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa kijijini kwake  Lupaso Masasi mkoani Mtwara.

 Wakuu  wa vyombo  vya Dola  wakikweka  shada la maua  kwenye kaburi la Hayati Rais B.W.Mkapa  baada ya kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na mjane wa Hayati B. Mkapa  mama Ana Mkapa na wanafamilia  baada ya   Mazishi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu hayati  Benjamin William Mkapa kijijini  Lupaso Masasi mkoani Mtwara.

Mabregedia Jenerali wa JWTZ wakibeba  Jeneza lenye Mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa kabla ya kushushwa kaburini Lupaso Masasi mkoani Mtwara.

Wakuu wa vyombo vya usalama nchini wakiweka shada la Maua kwenye kaburi la Rais mstaafu B.W.Mkapa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *