Taarifa kwa vyombo vya Habari

 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 30 Julai, 2020 amesafiri kwa gari kutoka Masasi Mkoani Mtwara hadi Jijini Dar es Salaam na kubaini kuwa sehemu ya barabara kuu ya kuanzia Lindi kwenda Dar es Salaam imeharibika kutokana na kutofanyika kwa matengenezo ipasavyo.
Mhe. Rais Magufuli ambaye akiwa njiani amesalimiana na wananchi wa Nangurukuru, Somanga, Rufiji, Kibiti na Mkuranga amesema barabara hiyo imeharibika kutokana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutowajibika ipasavyo katika utunzaji wake na hivyo ameahidi kuchukua hatua ili matengenzo yafanyike.
“Nimeshangazwa sana na ubovu huu wa barabara, hii sio barabara ambayo mimi niliiacha nikiwa Waziri wa Ujenzi, na tatizo kubwa hapa ni Wizara ya Ujenzi ambayo inashindwa kuitunza kwa kuhakikisha inafanyiwa matengenezo kwa wakati na inazuia upitishaji wa malori yanayobeba mizigo mizito kupita kiasi, ndugu zangu niacheni nifike ofisini, nitajua cha kufanya” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Alipofika Mto Rufiji, Mhe. Rais Magufuli amevuka Daraja la Mkapa lenye urefu wa meta 970.5 kwa miguu na kisha kukagua kibao cha ufunguzi wa daraja hilo uliofanywa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa tarehe 02 Agosti, 2003.
Ameeleza kuwa daraja hilo ni moja ya kumbukumbu ambazo Watanzania hasa waishio kusini hawatamsahau Hayati Benjamin William Mkapa kwa kuamua kutenga fedha na kujenga daraja refu kuliko yote ili kuondoa tatizo kubwa la usafiri lililosababishwa na kukatika kwa mawasiliano hasa wakati wa mvua.
Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli amewapa pole wananchi wa kusini kwa kuondokewa na mpendwa wao Hayati Benjamin William Mkapa ambaye jana aliongoza mazishi yake katika Kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara na ameahidi kuwa Serikali itamuenzi kwa kuendeleza mazuri yote aliyoyaanzisha.
Amewapongeza kwa maendeleo makubwa ambayo mikoa ya kusini imeyapata katika miaka ya karibuni, uzalishaji mzuri wa mazao na amewataka kuendelea kumuenzi Hayati Mkapa kwa kuchapa kazi na kujitegemea kama alivyosisitiza yeye mwenyewe kuwa mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kujiandaa kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu kwa kuchagua viongozi wazuri watakaowajibika kushughulikia kero zao na amewasisitiza kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano kabla, wakati na baada ya uchaguzi kama ilivyo desturi yao.
Akiwa Rufiji, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wa Wilaya ya Rufiji kushughulikia tatizo la mgogoro wa wakulima na wafugaji wanaoingiliana katika bonde la mto Rufiji, kushughulikia tatizo la maji na ameagiza gari la wagonjwa la Kituo cha Afya Rufiji litengenezwe ndani ya wiki 1.
Mjini Kibiti, Mhe. Rais Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi juu ya tatizo la soko la mji huo kukosa vyoo na amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kuhakikisha vyoo vinajengwa ndani ya siku 5 kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Akiwa Mkuranga, Mhe. Rais Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi juu ya mwekezaji anayedaiwa kutelekeza takribani ekari 1,750 za ardhi alizonunua kwa ulaghai kwa wananchi, ilihali wananchi wanahangaika kupata ardhi ya kuishi na kuendesha shughuli zao za uzalishaji mali, na Mhe. Rais Magufuli ameagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na viongozi wa Wilaya na Mkoa wa Pwani kushughulikia tatizo hilo pamoja na kuwasilisha kwake hati ya umiliki ili sehemu ya ardhi wapatiwe wananchi bure.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya kuimarisha majengo ya shule ya msingi Somanga Mkoani Lindi na amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya kutengeneza madawati ya shule ya Sekondari Ali Hassan Mwinyi iliyopo Mkuranga Mkoani Pwani.
Mhe. Rais Magufuli amewasili Jijini Dar es Salaam akitokea Masasi Mkoani Mtwara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *