TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza Majaji, Mahakimu na watumishi wa Mahakama hapa nchini kwa kuboresha huduma za Mahakama ikiwemo kuongeza kasi ya kupunguza mrundikano wa kesi Mahakamani ambao umekuwa ukisababisha usumbufu na gharama kubwa kwa wananchi.

Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 01 Februari, 2021 katika sherehe maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Sheria, Siku ya Sheria nchini na maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama Kuu zilizofanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma chini ya kauli mbiu isemayo “Miaka 100 ya Mahakama Kuu: Mchango wa Mahakama katika kujenga nchi inayozingatia uhuru, haki, udugu, amani na ustawi wa wananchi”.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na hatua kubwa za kuboresha Mahakama zilizopigwa katika miaka 5 iliyopita ambapo shilingi Bilioni 135 zilizotolewa na Serikali zimewezesha kuboreshwa kwa miundombinu ya Mahakama ikiwemo kujenga Mahakama Kuu za Kanda 3, Mahakama za Hakimu Mkazi 5, Mahakama za Wilaya 15, Mahakama za Mwanzo 18, Mahakama inayotembea (Mobile Court) ambayo imesikiliza Mashauri 778 na kuimarisha mifumo ya TEHAMA.

Mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi, kuteua Majaji wa Mahakama ya Rufani 17, kuteua Majaji wa Mahakama Kuu 52 (ambao wanafanya jumla ya Majaji kufikia 88) na kuajiri Mahakimu 396 (ambao wanafanya idadi ya Mahakimu kufikia 1,287).

Mhe. Rais Magufuli amesema juhudi hizo zimewezesha kuongezeka kwa kasi ya usikilizaji wa mashauri ambapo katika mwaka 2020 Mahakama za Mwanzo zilisikiliza mashauri 164,758 na kubakiwa na mrundikano wa mashauri 29 tu, Mahakama za Wilaya zilisikiliza mashauri 43,149 na kubakiwa na mrundikano wa mashauri 12 tu, Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi ilisikiliza mashauri 9 kati ya 11 na Mahakama ya Rufani ilisikiliza mashauri 1,216 na kubakiza mashauri 155 tu.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kueleza historia ya Mahakama tangu ilipoanzishwa hapa nchini miaka 100 iliyopita ambapo amesema wakati Tanganyika ikipata Uhuru mwaka 1961 Mhimili huo wa Dola ulikuwa umeshikiliwa na wakoloni kutokana na kutokuwepo kwa Majaji, Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama wa Kitanzania, na kwamba sura ya Mahakama inayoonekana leo imetokana na juhudi kubwa zilizofanyika baada ya Uhuru chini ya Marais wa Tanzania, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin William Mkapa, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa sasa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa vijana kujifunza historia ili kuelewa vizuri Taifa lilikotoka na juhudi kubwa zilizofanyika badala ya kuwasikiliza wanaosema Tanzania haijapiga hatua zozote tangu Uhuru, na kwamba hiyo ndio sababu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kulifanya somo la historia kuwa la lazima kwa wanafunzi.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameeleza kutoridhishwa kwake na kucheleweshwa kwa kesi za kodi zinazowahusu wafanyabiashara ambapo takwimu zinaonesha benki 4 kati takribani benki 50 zilizopo hapa nchini zimerekodi kesi 378 za kodi na mikopo zenye thamani ya shilingi Bilioni 738.99, hivyo ametoa wito kwa Mahakama kuharakisha maamuzi ya kesi hizo kwa kuwa zinaathiri uchumi na maendeleo.

Ametoa wito kwa Jaji Mkuu kuendelea kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya rushwa ambavyo bado vinafanywa na baadhi ya watumishi wa Mahakama kama ambavyo amechukua hatua dhidi ya watumishi 19 mwaka jana (2020), na amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ambao ni wenyeviti wa Kamati za Mahakama za Mikoa na Wilaya kuitisha vikao vya kamati hizo mara moja.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Majaji na Mahakimu wa Mahakama kutumia lugha ya Kiswahili katika uendeshaji wa mashauri yao ili kuiendeleza lugha hiyo na kuwarahisishia wananchi kuelewa, na kutokana na hilo amempongeza na kumpandisha cheo Mhe. Zepharine Nyalugenda Galeba kutoka Jaji wa Mahakama Kuu na kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani baada ya kutumia lugha ya Kiswahili kutoa hukumu kwenye kesi ya Mgodi wa North Mara dhidi ya Gerald Nzumbi.

Kwa upande wake, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali kutoa fedha kwa ajili ya maendeleo na uendeshaji wa shughuli za Mahakama ikiwemo kuboresha miundombinu, na kwamba juhudi hizo zinaendelea ambapo hivi sasa ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu katika Mikoa 6 (Mwanza, Arusha, Dodoma, Morogoro, Temeke na Kinondoni) unaendelea na pia ujenzi wa majengo 25 ya Mahakama za Wilaya unaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *