Monthly Archives: July 2020

HABARI PICHA MHE RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO AKIWA NJIANI KUREJEA DAR KUTOKA LUPASO MKOANI MTWARA KWENYE MAZISHI YA RAIS MSTAAFU B.W.MKAPA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wananchi wa Nangulukulu mkoani Lindi kuhusu ubovu wa barabara ya kutokea Lindi- Somanga wakati alipokuwa akitokea Msibani Masasi mkoani Mtwara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea zawadi ya Jogoo alilopewa na Mzee Shaweji Mohamed Kimbwembwe mkazi wa Somanga mkoani Lindi ambaye alifurahishwa na utendaji kazi wa Mhe. Rais Magufuli wa kuwaletea maendeleo Wananchi wanyonge.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na zawadi ya Jogoo alilopewa na Mzee Shaweji Mohamed Kimbwembwe mkazi wa Somanga mkoani Lindi ambaye alifurahishwa na utendaji kazi wa Mhe. Rais Magufuli wa kuwaletea maendeleo Wananchi wanyonge.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Somanga Rehema Mikidadi Ngenje Shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ukarabati wa Shule hiyo ya Msingi ya Somanga. Katika fedha hizo pia Rais aliagiza mwanafunzi huyo apewe Shilingi laki moja kutoka kwenye fedha hizo mara baada ya kuibua kero ya Shule hiyo

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Somanga Rehema Mikidadi Ngenje  akiwa ameshikilia Shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ukarabati wa Shule hiyo ya Msingi ya Somanga. Katika fedha hizo pia Rais aliagiza mwanafunzi huyo apewe Shilingi laki moja kutoka kwenye fedha hizo mara baada ya kuibua kero ya Shule hiyo, kushoto ni mwalimu wa shule hiyo Mariam Bakari.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono Wananchi wa Somanga mkoani Lindi mara baada ya kuwahutubia wakati akitokea Masasi mkoani Mtwara

Mzee Shaweji Mohamed Kimbwembwe mkazi wa Somanga mkoani Lindi akiliandaa Jogoo baada ya kumzawadia  Rais,  kwa kufurahishwa na utendaji kazi wa Mhe. Rais Magufuli wa kuwaletea maendeleo Wananchi wanyonge

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipita na kukagua Daraja la Mkapa linalopita katika Mto Rufiji mkoani Pwani wakati akitokea Masasi Mtwara kwenye msiba wa Marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa leo tarehe 30 Julai 2020. Daraja hilo linalounganisha Pwani na Mikoa ya Lindi na Mtwara lilijengwa na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa

 

Taarifa kwa vyombo vya Habari

 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 30 Julai, 2020 amesafiri kwa gari kutoka Masasi Mkoani Mtwara hadi Jijini Dar es Salaam na kubaini kuwa sehemu ya barabara kuu ya kuanzia Lindi kwenda Dar es Salaam imeharibika kutokana na kutofanyika kwa matengenezo ipasavyo.
Mhe. Rais Magufuli ambaye akiwa njiani amesalimiana na wananchi wa Nangurukuru, Somanga, Rufiji, Kibiti na Mkuranga amesema barabara hiyo imeharibika kutokana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutowajibika ipasavyo katika utunzaji wake na hivyo ameahidi kuchukua hatua ili matengenzo yafanyike.
“Nimeshangazwa sana na ubovu huu wa barabara, hii sio barabara ambayo mimi niliiacha nikiwa Waziri wa Ujenzi, na tatizo kubwa hapa ni Wizara ya Ujenzi ambayo inashindwa kuitunza kwa kuhakikisha inafanyiwa matengenezo kwa wakati na inazuia upitishaji wa malori yanayobeba mizigo mizito kupita kiasi, ndugu zangu niacheni nifike ofisini, nitajua cha kufanya” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Alipofika Mto Rufiji, Mhe. Rais Magufuli amevuka Daraja la Mkapa lenye urefu wa meta 970.5 kwa miguu na kisha kukagua kibao cha ufunguzi wa daraja hilo uliofanywa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa tarehe 02 Agosti, 2003.
Ameeleza kuwa daraja hilo ni moja ya kumbukumbu ambazo Watanzania hasa waishio kusini hawatamsahau Hayati Benjamin William Mkapa kwa kuamua kutenga fedha na kujenga daraja refu kuliko yote ili kuondoa tatizo kubwa la usafiri lililosababishwa na kukatika kwa mawasiliano hasa wakati wa mvua.
Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli amewapa pole wananchi wa kusini kwa kuondokewa na mpendwa wao Hayati Benjamin William Mkapa ambaye jana aliongoza mazishi yake katika Kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara na ameahidi kuwa Serikali itamuenzi kwa kuendeleza mazuri yote aliyoyaanzisha.
Amewapongeza kwa maendeleo makubwa ambayo mikoa ya kusini imeyapata katika miaka ya karibuni, uzalishaji mzuri wa mazao na amewataka kuendelea kumuenzi Hayati Mkapa kwa kuchapa kazi na kujitegemea kama alivyosisitiza yeye mwenyewe kuwa mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kujiandaa kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu kwa kuchagua viongozi wazuri watakaowajibika kushughulikia kero zao na amewasisitiza kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano kabla, wakati na baada ya uchaguzi kama ilivyo desturi yao.
Akiwa Rufiji, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wa Wilaya ya Rufiji kushughulikia tatizo la mgogoro wa wakulima na wafugaji wanaoingiliana katika bonde la mto Rufiji, kushughulikia tatizo la maji na ameagiza gari la wagonjwa la Kituo cha Afya Rufiji litengenezwe ndani ya wiki 1.
Mjini Kibiti, Mhe. Rais Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi juu ya tatizo la soko la mji huo kukosa vyoo na amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kuhakikisha vyoo vinajengwa ndani ya siku 5 kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Akiwa Mkuranga, Mhe. Rais Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi juu ya mwekezaji anayedaiwa kutelekeza takribani ekari 1,750 za ardhi alizonunua kwa ulaghai kwa wananchi, ilihali wananchi wanahangaika kupata ardhi ya kuishi na kuendesha shughuli zao za uzalishaji mali, na Mhe. Rais Magufuli ameagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na viongozi wa Wilaya na Mkoa wa Pwani kushughulikia tatizo hilo pamoja na kuwasilisha kwake hati ya umiliki ili sehemu ya ardhi wapatiwe wananchi bure.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya kuimarisha majengo ya shule ya msingi Somanga Mkoani Lindi na amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya kutengeneza madawati ya shule ya Sekondari Ali Hassan Mwinyi iliyopo Mkuranga Mkoani Pwani.
Mhe. Rais Magufuli amewasili Jijini Dar es Salaam akitokea Masasi Mkoani Mtwara.