Daily Archives: January 14, 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akutana na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad Ikulu Chato, mkoani Geita.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Seif Sharif Hamad leo tarehe 14 Januari, 2021 wamemtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli nyumbani kwake Chato Mkoani Geita na kufanya nae mazungumzo.

Wakizungumza na vyombo vya habari baada ya mazungumzo hayo, Mhe. Rais Mwinyi na Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Seif Sharif Hamad wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwakaribisha nyumbani kwake Chato na wameelezea kufurahishwa kwao na mazungumzo mazuri yaliyofanyika, yenye maslahi makubwa kwa Wazanzibar na Watanzania wote kwa ujumla.

Mhe. Rais Mwinyi ambaye ameongozana na Mkewe Mama Mariam Mwinyi amesema mazungumzo baina yao yalilenga kujenga nchi, kuwaunganisha zaidi Wazanzibar na amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa dhamira yake ya kuendelea kuisaidia Zanzibar ikiwemo ombi aliloliwasilisha hivi karibu kwa Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya Nje ya China Mhe. Wang Yi la kuomba fedha kiasi cha Dola za Marekani Milioni 75 kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 148 za barabara za Zanzibar.

“Kwa hivyo kwanza nianze kukushukuru wewe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utayari wako, wa kufanya kazi na sisi viongozi wa Zanzibar. Leo tupo hapa mimi na Maalim Seif Sharif Hamad tukiwa wamoja, tukiwa tunaongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa kule Zanzibar, na nataka niseme haya yasingewezekana kama tusingeungwa mkono nawe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu mara zote umekuwa mstari wa mbele kutaka Zanzibar iwe na umoja. Ukiwa kama Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, mara zote umekuwa ukiniunga mkono katika juhudi zetu za kuleta umoja kule Zanzibar. Leo tupo hapa tukiwa wamoja, tukiwa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na nataka nikuhakikishie kwamba sio sisi tu kama viongozi ndio tumeungana bali Wazanzibar wote wana muelekeo wa kuungana. Zile tofauti zetu za kisiasa tumeziweka pembeni, sasa hivi sote tunashirikiana katika kuijenga nchi yetu” amesema Mhe. Rais Mwinyi.

Kwa upande wake, Mhe. Seif Sharif Hamad amesema wamekuwa na mazungumzo mazuri ya namna ya kuwaunganisha Watanzania wote na kwamba amepata matumaini makubwa kuona Mhe. Rais Magufuli yupo pamoja na nao na ana dhamira ya kuwaunganisha Waunguja na Wapemba.

“Tulikuwa na mazungumzo mazuri, mazungumzo ya kidugu, na mazungumzo ambayo mimi yamenipa matumaini kwamba kiongozi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo pamoja na sisi, hasa katika suala zima la kuimarisha umoja, upendo na maelewano katika visiwa vya Unguja na Pemba, nimefarijika sana kumsikia yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais akituhakikishia kwamba yupo pamoja na sisi na anatuunga mkono kwa hali na mali, kwa hiyo Mhe. Rais nakushukuru sana. Lakini vile vile nimshukuru Rais wangu Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, nae vilevile tumekuwepo pamoja na kwa pamoja tumeweza kuchangia mawazo na nadhani kumsikia Mhe. Rais Magufuli kumetupa uzaidi sisi wa kuzidi kuwaunganisha Wazanzibari” amesema Mhe. Seif Sharif Hamad.

Aidha, Mhe. Seif Sharif Hamad ambaye wakati akitoka Mwanza kwenda Chato ameshuhudia ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi Mkoani Mwanza, amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo amesema litakuwa ukombozi na manufaa makubwa ya kijamii na kiuchumi sio tu kwa Watanzania bali pia nchi jirani.

Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi hao wa Zanzibar kwa kumtembelea nyumbani kwake Chato na pia amewapongeza wao na Wazanzibari wote kwa kuadhimisha miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Seif Sharif Hamad kwa kukubali kwake kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na kwamba kitendo hicho kimeonesha ukomavu wake katika uongozi na jinsi alivyoweka mbele maslahi ya Wazanzibari badala ya maslahi yake binafsi.

Mhe. Rais Magufuli amesema ana matumaini makubwa kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar itafanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii na amempongeza Mhe. Rais Mwinyi kwa kuanza vizuri uongozi wake ikiwemo kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuwashughulikia mafisadi.

Amewahakikishia viongozi hao kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na amesisitiza kuwa Watanzania wana kila sababu ya kuwa wamoja badala ya kuruhusu watu wenye maslahi yao binafsi kuwavuruga.

“Sitawaacha kamwe, na hasa kwa sababu wote kwa umoja wao wanahubiri amani, Rais wa Zanzibar Mhe. Mwinyi anahubiri amani, Maalim Seif anahubiri amani, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar anahubiri amani, Wazanzibari wote tuhubiri amani” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Viongozi wengine waliokuwepo ni Mawaziri, Makatibu Wakuu na viongozi wa Mkoa wa Geita.

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA RAIS MWINYI NA MAALIM SEIF IKULU, CHATO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad wakati wakiwa katika mazungumzo yao katika Ikulu ndogo ya Chato mkoani Geita leo tarehe 14 Januari 2021.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amewashika mikono Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad mara baada ya kuzungumza na Wanahabari katika Ikulu ndogo ya Chato mkoani Geita leo tarehe 14 Januari 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad mara baada ya mazungumzo yao katika Ikulu ndogo ya Chato mkoani Geita leo tarehe 14 Januari 2021.