Daily Archives: February 2, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 02 Februari, 2021 amemuapisha Mhe. Zephrine Nyalugenda Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Hafla ya kuapishwa kwa Mhe. Jaji Galeba imefanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, Katibu Mkuu Ikulu Dkt. Moses Kusiluka, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu na viongozi wa taasisi ambazo ni wadau wa karibu wa Mahakama.

Mhe. Galeba (aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu) ameapishwa baada ya kupandishwa cheo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni kutambua mchango wake wa kuthamini lugha ya Kiswahili ambapo alitumia lugha hiyo kutoa hukumu ya kesi ya mapitio namba 23/2020 kati mgodi wa dhahabu wa North Mara na mwananchi Gerald Nzumbi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Galeba kwa kupandishwa cheo na amemtaka kwenda kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu za Mahakama, na kwa kumtanguliza Mungu.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mahakama na Wizara ya Katiba na Sheria kufanya mabadiliko ya sheria na mifumo ya Mahakama iliyorithiwa kutoka kwa wakoloni na ambayo imesababisha hukumu za Mahakama kutolewa kwa lugha ya Kiingereza ambayo haifahamiki kwa Watanzania wengi, ili hukumu hizo zitolewe kwa lugha ya Kiswahili.

Amesema hoja za kuwa Kiswahili hakina misamiati ya kutosha hazina mashiko kwa kuwa mwaka 1999 timu ya Wanasheria iliandika kamusi ya sheria na pia lugha hiyo inatumiwa na watu wengi, Mataifa na taasisi mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari vya kimataifa.

Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na ucheleweshaji wa mambo unaofanywa na Wizara ya Katiba na Sheria na amemuagiza Waziri Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kufuatilia na kuhakikisha mchakato wa kuwaajiri watumishi 200 wa Mahakama ambao kibali cha kuajiriwa kwao kilishatoka wanaajiriwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Zepharine Nyalugenda Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzaia kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino leo Jumanne Februari 2, 2021