Monthly Archives: March 2021

RAIS MHE. SAMIA SULUHU HASSAN ASHUHUDIA MAKAMU WA RAIS AKIAPA IKULU YA CHAMWINO MKOANI DODOMA.

Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 31 Machi, 2021 ameapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Dkt. Mpango ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika hafla iliyofanyika Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu, Mawaziri na Naibu Mawaziri na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Wengine ni Mawaziri Wakuu wastaafu (Mhe. John Samwel Malecela na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda), Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Ndg. Philip Mangula, Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Wabunge, viongozi wa Dini na viongozi wa taasisi mbalimbali.

Akizungumza baada ya kiapo hicho, Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Dkt. Mpango kwa kushika wadhifa huo wa Makamu wa Rais na ameeleza kuwa baada ya kupitia majina mbalimbali ameona Dkt. Mpango anafaa kushika wadhifa huo kutokana na uchapakazi wake, umahiri, ucha Mungu na utulivu.

Amebainisha kuwa kutokana na sifa hizo anatarajia pamoja na majukumu mengine Dkt. Mpango atamsaidia katika uchumi, udhibiti wa fedha za Serikali na kwa kuwa masuala ya Muungano yapo katika Ofisi yake atashughulikia ajenda iliyokwama ya uhusiano wa kifedha katika Muungano.

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Mpango amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa imani yake kwake na ameahidi kuwa atakuwa msaidizi mwaminifu na mtiifu kwa Mhe. Rais na nchi ya Tanzania.

Ameongeza kuwa yupo tayari kuchapakazi mchana na usiku, kushirikiana na viongozi wengine na amesisitiza kuwa Watanzania hawana hofu na uongozi wa Mhe. Rais Samia.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai na Jaji na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wamempongeza Mhe. Dkt. Mpango kwa kushika wadhifa huo na wameahidi kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFANYA MABADILIKO YA BARAZA LA MAWAZIRI NA KUTEUA WABUNGE 3

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 31 Machi, 2021 amefanya uteuzi wa Wabunge 3 na kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambapo amewabadilisha wizara baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri na ameteua Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya.

Mhe. Rais Samia amefanya uteuzi wa Wabunge 3 ambao ni 

 • Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Kabla ya uteuzi huu alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi)
 • Mhe. Balozi Liberata Mulamula
 • Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk

Mhe. Rais Samia amemteua Mhe. Balozi Hussein Athuman Katanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Balozi Katanga alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan.

Baada ya mabadiliko, ifuatayo ni orodha ya Baraza la Mawaziri.

Ofisi ya Rais.

 • Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
 • Waziri – Mhe. Ummy Ali Mwalimu 

(Kabla ya uteuzi huu alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira).

 • Naibu Mawaziri – Mhe. Dkt. Festo John Dugange
 • Naibu Waziri – Mhe. David Silinde
 • Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
 • Waziri – Mhe. Mohammed Omar Mchengerwa
 • Naibu Mawaziri – Mhe. Deogratius Ndejembi

Ofisi ya Makamu wa Rais.

 • Muungano na Mazingira
 • Waziri – Mhe. Selemani Jafo

(Kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa TAMISEMI)

 • Naibu Waziri – Mhe. Hamad Hassan Chande

Ofisi ya Waziri Mkuu.

 • Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
 • Waziri – Jenister Joakim Mhagama
 • Naibu Mawaziri – Mhe. Patrobas Katambi
 • Naibu Waziri – Mhe. Ummy Nderiananga
 • Uwekezaji
 • Waziri – Mhe. Geofrey Mwambe (Kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara)
 • Naibu Waziri – Mhe. William Tate Ole Nasha

Wizara

 • Wizara ya Fedha na Mipango
 • Waziri – Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria)
 • Naibu Waziri – Mhe. Hamad Yussuf Masauni
 • Wizara ya Katiba na Sheria.
 • Waziri – Mhe. Prof. Palamagamba Aidan Kabudi (Kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki)
 • Naibu Waziri – Mhe. Geofrey Mizengo Pinda
 • Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
 • Waziri – Mhe. Elias Kwandikwa
 • Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
 • Waziri – Mhe. Balozi Liberrata Mulamula
 • Naibu Waziri – Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk
 • Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
 • Waziri – Mhe. George Simbachawene
 • Naibu Waziri – Mhe. Khamis Hamza
 • Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
 • Waziri – Mhe. Leonard Chamriho
 • Naibu Waziri – Mhe. Geofrey Kasekenya
 • Naibu Waziri – Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara
 • Wizara ya Viwanda na Biashara.
 • Waziri – Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Uwekezaji)
 • Naibu Waziri – Mhe. Exaud Kigahe
 • Wizara ya Madini.
 • Waziri – Mhe. Dotto Mashaka Biteko
 • Naibu Waziri – Mhe. Shukrani Manya
 • Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
 • Waziri – Mhe. William Lukuvi
 • Naibu Waziri – Mhe. Dkt. Angelina Mabula
 • Wizara ya Maji
 • Waziri – Mhe. Jumaa Hamidu Aweso
 • Naibu Waziri – Mhe. MaryPrisca Mahundi
 • Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo
 • Waziri – Mhe. Innocent Bashungwa
 • Naibu Waziri – Mhe. Pauline Gekul (Kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Waziri wa Mifugo na uvuvi)
 • Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
 • Waziri – Mhe. Prof. Joyce Ndalichako
 • Naibu Waziri – Mhe. Omar Kipanga
 • Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
 • Waziri – Mhe. Dorothy Gwajima
 • Naibu Waziri – Mhe. Godwin Mollel
 • Naibu Waziri – Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Waziri wa Fedha)
 • Wizara ya Nishati
 • Waziri – Mhe. Dkt. Medard Matogolo Kalemani
 • Naibu Waziri – Mhe. Stephen Byabato
 • Wizara ya Maliasili na Utalii.
 • Waziri – Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro
 • Naibu Waziri – Mhe. Mary Francis Masanja
 • Wizara ya Kilimo.
 • Waziri – Mhe. Prof. Adolf Mkenda
 • Naibu Waziri – Mhe. Hussein Mohammed Bashe
 • Wizara wa Mifugo na Uvuvi.
 • Waziri – Mhe. Mashimba Mashaka Ndaki
 • Naibu Waziri – Mhe. Abdallah Khamis Ulega (Kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo)
 • Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
 • Waziri – Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile
 • Naibu Waziri  – Mhe. Kundo Mathew

Katibu Mkuu Kiongozi, Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya na waliobadilishiwa wizara wataapishwa kesho saa 9:00 Alasiri Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.

Aidha, Mhe. Rais Samia ametoa miezi 3 kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Naibu Waziri wake kuanzisha wizara hiyo vinginevyo watahesabiwa kuwa wameshindwa kufanya majukumu yao.

Mhe. Rais Samia amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri hao kwenda kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kwamba watakaoshindwa kutimiza wajibu wao hatosita kufanya mabadiliko.