Daily Archives: April 17, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 17 Aprili, 2021 ametunuku Kamisheni kwa Maafisa wapya 393 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Nchi rafiki ambao wamehitimu mafunzo katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli Mkoani Arusha (TMA) na nje ya Nchi.
Kati ya Maafisa hao, Maafisa 143 wa JWTZ wamehitimu mafunzo ya 1 ya Shahada ya 1 ya Sayansi ya Kijeshi iliyoanzishwa kwa ushirikiano wa TMA na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Maafisa 233 wa JWTZ wamehitimu kozi ya mwaka mmoja na Maafisa 7 kutoka Nchi rafiki za Eswatini na Kenya wamehitimu kozi ya mwaka mmoja.
Maafisa wapya wa JWTZ waliotunikiwa Kamisheni baada ya kuhitimu mafunzo nje ya Nchi wamepata mafunzo hayo katika nchi za Burundi, China, India, Kenya, Morocco, Ujerumani na Marekani.
Mhe. Rais Samia amewatunuku Maafisa hao cheo cha Luteni Usu na pia ametoa zawadi kwa Maafisa wapya waliofanya vizuri zaidi katika mafunzo ya jumla, darasani, medani na mwanamke aliyefanya vizuri zaidi.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewatunuku Shahada ya 1 ya Sayansi ya Kijeshi Maafisa 143 waliohudhuria kozi hiyo ambayo imetolewa kwa mara ya kwanza kwa ushirikiano wa Chuo cha TMA na Chuo cha IAA.
Mkuu wa Chuo wa TMA Brig. Jen. Jackson Jailos Mwaseba amesema mafunzo hayo yalianza mwaka 2017 ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa JWTZ wa kutoa Shahada ya Sayansi ya Kijeshi na kwamba ifikapo mwaka 2024 TMA itaanza kutoa mafunzo ya shahada pasipo kushirikiana na chuo chochote baada ya taratibu kukamilika.
Pamoja na kutunuku Kamisheni na Shahada kwa Maafisa wapya wa JWTZ, Mhe. Rais Samia ameipongeza TMA na IAA kwa ubunifu wa kuanzisha mafunzo hayo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa Serikali kutoa shilingi Bilioni 2 zilizotumika kujenga uwanja wa maadhimisho ya Kitaifa uliopo Ikulu Chamwino ambao umetumika kwa mara ya kwanza katika utoaji wa Kamisheni kwa Maafisa wapya wa Jeshi na ambao utatumika kwa matukio mengine mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Jen. Mabeyo ameishukuru Serikali kwa jinsi ambavyo imekuwa bega kwa bega na JWTZ na amemhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa Jeshi lipo imara kulinda mipaka ya nchi, wananchi na rasilimali za Tanzania.
Amewataka Maafisa wapya waliotunukiwa Kamisheni leo kuheshimu, kuthamini, kuzingatia na kutunza viapo vyao katika maisha yao yote kwani viapo hivyo ndivyo vinaunda sheria ya ulinzi.
Jen. Mabeyo ameeleza kusikitishwa kwake na vijana 854 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao wamekiuka taratibu kwa kuanzisha mgomo na kufanya maandamano ya kwenda Ikulu kwa madai ya kutaka kumuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu ili wadai kuandikishwa Jeshini kama walivyoahidiwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Vijana hao ni kati ya vijana 2,400 walioahidiwa kuandikishwa Jeshini na walifanya uamuzi huo baada ya Jeshi kuamua kuwapunguza katika kazi ya ujenzi wa Ikulu Chamwino baada ya kazi kupungua ili waende kufanya katika kazi maeneo mengine, lakini wao wakapinga kwa madai wangekosa kuandikishwa Jeshini.
Jen. Mabeyo amesema Jeshi halikuwa na lengo hilo na limelazimika kusitisha mikataba yao kwa kuwa kosa walilolifanya ni sawa na uasi na kwamba halivumiliki. Ameongeza kuwa pamoja na kufanya uchunguzi zaidi wa kwa nini walifanya hivyo Jeshi limeamua kutafakari upya mpango wa kuchukua vijana wa kujitolea kwa ajili ya kujiunga na JKT.

RAIS NA AMIRI JESHI MKUU MHE. SAMIA SULUHU HASSAN ATUNUKU KAMISHENI KWA MAAFISA WANAFUNZI WA JESHI LA WANANCHI WA TANZANIA (JWTZ) KATIKA VIWANJA VYA IKULU CHAMWINO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akitoka kukagua Gwaride Maalumu lililoandaliwa na Maafisa Wanafunzi 143 kundi la 01/17 kabla ya kuwatunuku Kamisheni katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 17 Aprili, 2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwatunuku Kamisheni Maafisa Wanafunzi 143 kundi la 01/17 katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma
Maafisa Wanafunzi 143 kundi la 01/17 wakivalishana vyeo mara baada ya kutunukiwa Kamisheni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.