Daily Archives: May 3, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 03 Mei, 2021 amefanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) Bi. Kristalina Georgieva kuhusu ushirikiano kati Tanzania na IMF katika masuala ya kiuchumi.
Mhe. Rais Samia aliyekuwa ofisini kwake (Ikulu Chamwino) Mkoani Dodoma amemshukuru Bi. Kristalina aliyekuwa nchini Marekani kwa ushirikiano na ufadhili mkubwa ambao IMF umeutoa nchini Tanzania na amemhakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano huo kwa lengo la kuendelea kujenga uchumi imara wa Tanzania.
Amemueleza juu ya hali ya uchumi wa Tanzania kwa sasa ambapo ukuaji wake umeshuka kutoka wastani wa asilimia 6.9 mwaka jana hadi asilimia 4.7 hivi sasa kutokana na changamoto za janga la Korona (Covid-19) ambalo limeathiri sekta za uzalishaji na huduma za kijamii zikiwemo utalii, afya na kilimo.
Mhe. Rais Samia amesema japo kuwa hali ya uchumi wa Tanzania bado ni nzuri, Serikali inahitaji kushirikiana zaidi na IMF kunusuru sekta zilizoathirika na janga la Korona na kuendeleza miradi ya kimkakati ambayo utekelezaji wake unaendelea ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere katika mto Rufiji utakaozalisha megawati 2,115, ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway) na ujenzi wa barabara na madaraja.
Amesema pamoja na kukabiliwa na changamoto hizo, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha uchumi ikiwemo kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara kama vile kuondoa dosari za kikodi na ardhi, kuimarisha utawala bora na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya nchi.
Kwa upande wake Bi. Kristalina amempa pole Mhe. Rais Samia kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, amempongeza kwa kupokea kijiti cha Urais na amemhakikishia kuwa IMF ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wake na Tanzania kwa lengo la kuimarisha uchumi.
Bi. Kristalina amesema IMF ipo tayari kutoa ufadhili wa haraka kwa Tanzania kwa ajili ya kusaidia maeneo yaliyopata madhara makubwa ya kiuchumi kutokana na janga la Korona zikiwemo sekta za utalii, afya, uzalishaji na huduma za kijamii na amebainisha kuwa shirika hilo litafanyia kazi mara moja maombi ya mkopo nafuu kutoka Tanzania.
Ameongeza kuwa katika awamu ya pili, IMF imepanga kutumia Dola za Marekani Bilioni 650 kwa ajili ya kusaidia kwa dharura uchumi wa nchi mbalimbali zikiwemo nchi zinazoendelea zilizopatwa na madhara ya Korona.
Kufuatia ahadi hiyo, Mhe. Rais Samia amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ambao wamehudhuria katika mazungumzo hayo kukamilisha haraka mchakato wa maandiko ya kuomba mkopo nafuu kutoka IMF ili fedha hizo zisaidie kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijamii.

MHE RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS MSTAAFU WA NIGERIA MHE OLESEGUN OBASANJO IKULU CHAMWINO LEO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 03 Mei, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe. Olusegun Obasanjo.
Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma ambapo Mhe. Rais Mstaafu Obasanjo ametoa salamu zake za rambirambi kwa Mhe. Rais Samia kufuatia vifo vya waliokuwa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni Hayati Benjamin William Mkapa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli waliofariki dunia tarehe 23 Julai, 2020 na tarehe 17 Machi, 2021 mtawalia.
Mhe. Rais Mstaafu Obasanjo amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kupokea kijiti cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na amemtakia heri katika majukumu yake.
Aidha, katika mazungumzo hayo viongozi hao wamezungumzia hali ya usalama Barani Afrika na umuhimu wa Wakuu wa Nchi kujadiliana na kutafuta suluhisho la migogoro hiyo ambayo inasababisha vifo vya watu wasio na hatia hasa wanawake na watoto.
Pia viongozi hao wamezungumzia masuala ya maendeleo hasa katika uchumi na kusisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuongeza ushirikiano na kuondoa vikwazo vya biashara na uwekezaji.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika Mazungumzo na Rais mstaafu wa Nigeria Mhe. Olesegun Obasanjo Ikulu Chamwino leo Tarehe 03 Mei 2021.

Rais mstaafu wa Nigeria Mhe. Olesegun Obasanjo akizungumza na wanahabari mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na Mwenyeji wake Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu Chamwino leo Tarehe 03 Mei 2021.