Monthly Archives: June 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 30 Juni, 2021amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) Bw. Wamkele Mene,  Ikulu Chamwino, Mkoani Dodoma.

Mhe. Rais Samia amempongeza Bw. Wamkele kwa kushinda nafasi  ya Ukatibu Mtendaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) na kumhakikishia kuwa Tanzania itashirikiana nae katika kufanikisha utendaji kazi wake katika kulikwamua Bara la Afrika Kiuchumi. Aidha, Mhe. Rais amemhakikishia kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho za kuridhia Mkataba wa AfCFTA.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa AfCFTA Bw. Wamkele Mene amempongeza Mhe. Samia kuwa Rais wa kwanza Mwanamke nchini Tanzania na Rais pekee mwanamke ambaye ni Mkuu wa Nchi na Serikali Barani Afrika.

Bw. Wamkele ameshukuru kuwa Tanzania imerejea kwenye majadiliano na masuala mengi waliojadili wamekubaliana.

Aidha, Bw. Wamkele amemualika Mhe. Rais Samia kuhudhuria mkutano wa Sekretarieti na kuwaMzungumzaji Mkuu kwenye mkutano huo wenye lengo la kuandaa Itifaki ya Wanawake katika Biashara (Women in Trade Protocol ) utakaofanyika Jijini Accra nchini Ghana kwa ajili ya Wafanyabiashara ndogondogo. Kupitia mkutano huo Sekretarieti inatarajia kufanya harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya kuwezesha biashara kutoka taasisi mbalimbali za fedha zikiwemo benki. 

Bw. Wamkele amemhakikishia Mhe. Rais kuwa Sekretarieti ya AfCFTA inakusudia kuhakikisha wanachama wake wote wananufaika kwa usawa kupitia uwekezaji katika viwanda ambavyo vitaongeza minyororo ya thamani ya bidhaa zinazozalishwa katika nchi wanachama.

Katibu Mtendaji wa AfCFTA amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kuirudisha Tanzania katika dhima yake ya uongozi kama  alivyowahi kufanya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa muasisi wa Umajumui wa Afrika (Pan Africanism).​

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Akutana na Kuzungumza na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AFCTA) Mhe. Wamkele Mene, Ikulu Chamwino Jijini Dodoma leo tarehe 30 Juni, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mhe. Wamkele Mene Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AFCTA) Ikulu Chamwino Jijini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Mhe. Wamkele Mene Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AFCTA) Ikulu Chamwino Jijini Dodoma.