Daily Archives: July 2, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 02 Julai, 2021 amewaongoza viongozi mbalimbali na waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale.

Shughuli za kuaga mwili wa Mhandisi Mfugale zimefanyika katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Katanga, Katibu Mkuu Kiongozi-Zanzibar Mhandisi Zena Said pamoja na viongozi wengine wa  Taasisi za Umma na Binafsi.

Mhe. Rais Samia amesema kifo cha Mhandisi Mfugale kimeacha simanzi na pengo kubwa kwa familia, Serikali na Taifa kwa ujumla.

Amesema Serikali imepoteza mtumishi na kiongozi mwadilifu, makini, shupavu na mchapakazi hodari. Taifa limepoteza Mhandisi mahiri na mzalendo wa kweli ambaye daima alikuwa tayari kuitumikia nchi kwa moyo wake wote.

Mhe. Rais Samia amesema Mhandisi Mfugale ameacha alama kubwa kwa nchi kwa kuwa amekuwa mtumishi wa umma kwa takriban miaka 45, tangu mwaka 1977 ambapo ameongoza TANROADS kwa takriban miaka 12 tangu mwaka 2009. Katika kipindi hicho Mhandisi Mfugale ametoa mchango mkubwa kwa nchi hususan katika sekta ya miundombinu ya barabara na madaraja.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Mhandisi Mfugale atakumbukwa kwa kubuni na kusimamia ujenzi wa Daraja la Umoja (Mtambaswala)  linalounganisha Tanzania na Msumbiji, Daraja la Nyerere (Kigamboni), Daraja la Mkapa katika Mto Rufiji, Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi, Daraja la Magufuli katika Mto Kilombero, Daraja la Mfugale (TAZARA), Daraja la Kijazi (Ubungo), Daraja la Tanzanite (Selander), Daraja la Kigongo – Busisi (JPM), na Miradi mingi ya kimakakati.

Mhe. Rais Samia amesema kutokana na mchango mkubwa alioutoa Mhandisi Mfugale kwa Taifa, kila mmoja wetu anapaswa kutumia fursa aliyopewa kuacha alama ili nchi ipate maendeleo kwa haraka.

Mhandisi Mfugale alifariki dunia Juni 29, 2021 katika hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.

“Bwana ametoa, Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe”

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Aongoza Viongozi na Wananchi Kuaga Mwili wa Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Marehemu Mhandisi Patrick Mfugale katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam Leo Tarehe 02 Julai, 2021.

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisaini kitabu cha rambirambi alipohudhuria ibada ya kuaga mwili wa marehemu Mhandisi Patrick Mfugale katika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam leo tarehe 02 Julai, 2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akitoa Heshima za mwisho katika Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa  Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale katika viwanja wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia waombolezaji wakati wa ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa  Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale katika viwanja wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akitoa pole kwa familia ya aliyekuwa  Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale katika viwanja wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.