Daily Archives: July 6, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 06Julai, 2021 amezungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mhe.Antony Blinken.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mhe.Blinken amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kushika hatamu ya uongozi nchini na kumhakikishia kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuleta maendeleo kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa kuzingatia vipaumbele vya nchi.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Blinken amepongeza Mhe. Rais Samia kwa hatua anazozichukua katika kukabiliana na ugonjwa  wa Corona nchini Tanzania na Marekani ipo tayari kuisaidia Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Aidha, Mhe. Blinken amepongeza  jitihada za Mhe. Rais Samia katika kuimarisha Demokrasia nchini ikiwa ni pamoja na azma yake ya kukutana na kushirikiana na Vyama vya Siasa  pamoja na kusimamia Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Pia amepongeza uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na kuahidi kuwa hali hiyo imeivutia Marekani kushawishi wawekazaji wake kuja kuwekeza nchini.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia ameshukuru kwa pongezi na kuahidi kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana naSerikali ya Marekani kukuza uhusiano baina ya nchi hizi mbili katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa. 

Aidha, Mhe. Rais Samia ametoa mwaliko kwa  Rais wa Marekani Mhe. Joseph Biden  kutembelea Tanzania ili kuzidi kuimarisha uhusino uliopo kati ya nchi hizi mbili.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Azungumza kwa Simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwa njia ya Simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mhe. Antony Blinken, leo tarehe 06 Julai, 2021 Ikulu Jijini Dodoma ambapo kwenye mazungumzo yao Waziri huyo amemhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kukuza ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika Nyanja mbalimbali za maendeleo.