Daily Archives: September 7, 2021

Ziara ya Royal Tour ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika Mikoa ya Arusha na Mara tarehe 06 Septemba, 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wananchi wa Karatu Mkoani Arusha alipokua njiani akielekea Ngorongoro kwa ajili kurekodi kipindi maarufu cha Royal Tour kitakachotangaza Utalii, Biashara na Uwekezaji Nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wananchi wa Serengeti Mkoani Mara alipowasili kwa ajili kurekodi kipindi maarufu cha Royal Tour kitakachotangaza Utalii, Biashara na Uwekezaji Nchini.
Wananchi wa Serengeti Mkoani Mara waliojitokeza kumsikiliza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alipowasili kwa ajili kurekodi kipindi maarufu cha Royal Tour kitakachotangaza Utalii, Biashara na Uwekezaji Nchini.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 06 Septemba, 2021 amewasili katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara akiwa na kundi la wapiga picha wa  kipindi cha Royal Tour kwa ajili ya kuendelea kuonesha na kuelezea vivutio vya utalii vilivyopo nchini kupitia filamu itakayoandaliwa na timu hiyo.

Mhe. Rais Samia amewaambiwa wananchi wa Wilaya hiyo waliojitokeza kumpokea kuwa filamu hiyo itakapokamilika itatangaza maeneo yote yenye vivutio vya utalii nchini na kuchochea uchumi wa nchi kupitia watalii, wawekezaji na wafanyabiashara.

Aidha, Mhe. Rais amesema filamu hiyo  pia itaelezea hali halisi ya siasa zilivyo nchini tofauti na baadhi ya mataifa mengine inavyoelezea.

Amesema kwa sasa wahisani wengi wametoka katika utoaji wa misaada na kujikita katika biashara, hivyo filamu hiyo itasaidia kueleza na kuonesha maeneo mbalimbali ya utalii ambayo yatatoa furza za biashara na uwekezaji.

Pia, Mhe. Rais Samia amewahakikishia wananchi wa Wilaya  ya Serengeti kuwa ahadi zote zilizotolewa na Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 zitatekelezwa.