Daily Archives: September 11, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 11 Septemba, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bi. Amina J. Mohammed, Ikulu Chamwino, Mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Bi. Amina amewasilisha salamu kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na kumpongeza Mhe. Rais Samia kwa kushika nafasi ya Urais na kumtakia heri katika majukumu yake.

Mhe. Amina amemuhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kumuunga mkono katika jitihada zake mbalimbali za kuiletea maendeleo Tanzania , ikiwemo kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Aidha, amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada anazochukua dhidi ya janga la UVIKO 19 ambapo amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kuhakikisha kuwepo na usawa wa upatikanaji wa chanjo na wanaendelea na majadiliano na Taasisi za Kifedha kuona ni jinsi gani zinasadia nchi zinazoendelea kukabiliana na ugonjwa huo.

Vilevile, ameahidi kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Amina kwa kuteuliwa tena kushika nafasi hiyo ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kumhakikishia ushirikiano zaidi kwa kuwa Umoja wa Mataifa kupitia taassisi zake mbalimbali ni mbia wa maendeleo nchini.

Mhe. Rais Samia amemueleza Mhe. Amina kuwa Serikali  inaendelea kuboresha mazingira bora ya biashara na uwekezaji nchini ambapo katika kipindi cha miezi mitatu idadi ya wawekezaji imeongezeka.

Mhe. Samia Suluhu Hassan Akutana na Kuzungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bibi Amina J. Mohammed Ikulu Chamwino, Jijini Dodoma Leo tarehe 11 Septemba, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bibi Amina J. Mohammed wakati Bibi Amina alipofika Ikulu Chamwino, Jijini Dodoma leo tarehe 11 Septemba, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bibi Amina J. Mohammed wakati Bibi Amina alipofika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bibi Amina J. Mohammed baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao, Ikulu Chamwino Jijini Dodoma.