Daily Archives: September 13, 2021

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Awaapisha Viongozi Mbalimbali Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma Leo Tarehe 13 Septemba, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Makame Mbarawa (Mb) kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Januari Yusuf Makamba (Mb) kuwa Waziri wa Nishati

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. Stergomena Tax kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Viongozi mbalimbali walioteuliwa Wakila Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma katika hafla iliyofanyika katika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 13 Septemba 2021. Kutoka kulia ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Nishati Januari Yusuf Makamba (Mb) Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax (Mb), pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali mara baada ya tukio la Uapisho lililofanyika katika viwanja vya Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kuwapanga upya Wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga, bila kutumia nguvu ili wafanye biashara zao kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Mhe. Rais Samia ametoa agizo hilo leo mara baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua jana tarehe 12 Septemba, 2021 katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma.

Mhe. Rais amesema Serikali ilitoa fursa kubwa kwa Wamachinga kufanya biashara za kujipatia kipato kwa uhuru lakini wametumia fursa hiyo vibaya na kufanya biashara kiholela ambapo baadhi yao hupanga bidhaa nje ya maduka na kuwazuia wenye maduka kufanya biashara, kitendo ambacho kinaikosesha Serikali kodi toka kwa wafanyabiashara hao.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka viongozi aliowaapisha na walio katika nafasi mbalimbali za uongozi kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa kuwa mabadiliko aliyofanya katika Baraza la Mawaziri ni ya kawaida lakini ni endelevu.

Mhe. Rais Samia amewataka watendaji Serikalini kuendesha shughuli zao kwa vitendo ili kuwaletea wananchi maendeleo  na si kwa maneno makali ambayo  hayana tija kwa maendeleo ya wananchi.

Awali, Mhe. Rais Samia amemuapisha Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Prof.Makame Mnyaa Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. January Yusuf Makamba, kuwa Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Dkt.Stergomena Lawrence Tax, kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya Siasa.