Daily Archives: September 14, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 14 Septemba, 2021 amezindua Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Akizungumza kabla ya kuzindua Mkakati huo, Mhe. Rais Samia amesema Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwaka 2022 ina lengo la kufahamu idadi ya watu, mahali walipo, jinsia, rika, elimu, ajira, shughuli, makazi yao, mahali yalipo na hali yake.

Mhe. Rais Samia amesema taarifa hizo zitasaidia kufahamu wastani wa ongezeko la idadi ya watu katika nchi na pia hali ya uhamiaji kutoka vijijini kwenda mijini na kuwezesha nchi kutambua hatua mbalimbali za kimaendeleo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Sensa inasaidia Serikali kufanya maamuzi kuhusu ugawaji wa rasilimali za Taifa na kupeleka huduma mbalimbali za jamii kwa wananchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu kwenye maeneo yao kulingana na idadi ya watu na mahitaji.

Pia amesema mbali na kuwa kupitia madodoso ya Sensa ya mwaka 2022, Sensa hiyo itawezesha kutambua idadi ya majengo na mahali yalipo, itawezesha kufahamu hali ya mahitaji ya makazi nchini na kufahamu na kupanga mitaa kupitia anuani za makazi ambazo zitachochea benki kutoa mikopo na kupunguza viwango vya riba.

Mhe. Rais amewaomba viongozi wa Serikali, Dini na vyama vya siasa  kusisitiza wananchi kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo la Sensa  ya Watu na Makazi. Pia amewasihi viongozi hao Dini wasisahau kuzungumzia sula la Sensa kila watakapokuwa wakitoa mahubiri kwa waumini wao.

Mhe. Rais Samia ameishukuru na kuipongeza Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa kwa kukamilisha mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji Sensa mapema na kuwataka kwenda kuutekeleza.

Tukio hilo la uzinduzi limehudhuriwa pia na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Dkt. Khalid Salim Mohamed, Mawaziri, Manaibu Mawaziri, viongozi wa Dini pamoja na  vyama vya siasa.

Mhe. Rais Samia Azindua Mkakati wa Elimu ya Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Leo Tarehe 14 Septemba, 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akibonyeza kitufe kuzindua rasmi Mpango wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, leo tarehe 14 Septemba, 2021 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akilihutubia Taifa katika Hafla ya  uzinduzi rasmi wa Mpango wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 leo tarehe 14 Septemba, 2021 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma. 
Wananchi wa Dodoma wakishangilia mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwasili katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma leo tarehe 14 Septemba, 2021 kwa ajili ya kuzindua Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022.

Msanii wa Bongo Flavour Ali Kiba akitumbuiza katika tukio la uzinduzi wa Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 lililofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Msanii wa Bongo Flavour Nandy akitumbuiza katika tukio la uzinduzi wa Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 lililofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Msanii wa Bongo Flavour Diamond Platnumz akitumbuiza katika tukio la uzinduzi wa Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 lililofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.