Daily Archives: September 15, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 15 Septemba, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Sudan ya Kusini Salva Kiir Mayardit, Balozi Albino Ayuel Aboug, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Balozi Aboug amesema ujumbe huo pamoja na mambo mengine, Mhe. Rais Salva Kiir Mayardit ametaka kuimarishwa zaidi kwa uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na Sudan Kusini.

Amesema Sudan Kusini inaomba kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo yake na pia kununua  chakula kutoka Tanzania.

Aidha, Balozi Aboug amesema Sudan Kusini pindi Reli ya Kisasa (SGR) itakapokamilika ingependa kusafirishia bidhaa zake kupitia reli hiyo.

Pia, amesema Sudan Kusini bado inahitaji kupata walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili kuanzia ngazi ya shule za msingi kutoka nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia amemhakikishia mjumbe huyo kuwa Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano na uhusiano uliopo kwa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kuhusu ombi la kutumia Bandari ya Dar es Salaam, Mhe. Rais Samia amemhakikishia mjumbe huyo kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Sudan Kusini kutumia Bandari ya Dar es Salaam katika kukuza uchumi wa nchi zote mbili.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewaomba wanawake nchini kushikamana ili kuhakikisha wanamchagua mwanamke kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe 15 Septemba, 2021 wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya  Siku ya Kimataifa ya Demokrasia iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam iliyokuwa na kaulimbiu “Ajenda ya Mwanamke ni Turufu ya Ushindi

Amesema kwa sasa Rais aliyepo madarakani amewekwa kwa kudra ya Mungu na matakwa ya Katiba hivyo amewaomba wanawake kuhakikisha kuwa mwaka 2025 wanamuweka madarakani Rais mwanamke.

Mhe. Rais Samia amewataka wanawake kuhakikisha fadhila walizopewa na Mungu hawaziachii kwa kuwa wanawake wamefanya kazi kubwa ya kuleta uhuru, kujenga siasa na kuwabeba wanaume katika siasa za nchi, hivyo iwapo wataziachia fadhila hizo Mungu atawalaani.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongozwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia kama inavyotamkwa wazi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 3 (1).

Pia amesema Tanzania inaongoza kwa Uhuru wa vyombo vya Habari kwa kuwa na vyombo vingi vya habari ambavyo kati ya hivyo asilimia 75 vinamilikiwa na watu binafsi.

Vilevile, amesema Serikali ya Awamu ya Sita itajitahidi kushughulikia masuala ya haki za wanawake na usawa wa jinsia ili kukuza demokrasia nchini, ikiwemo kutekeleza yaliyomo kwenye Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.

Mhe. Rais Samia amesema Demokrasia inahusiana kwa karibu na masuala ya haki ya kuishi hivyo wananchi wachukue tahadhari dhidi ya UVIKO 19 kwa kupata chanjo kwa hiyari ili kupunguza madhara yatokanayo na janga hilo ikiwa ni pamoja na vifo.

Katika maadhimisho hayo, Mhe. Rais Samia amekabidhiwa Tuzo kama kiashiria cha ushindi wa mwanamke Mtanzania iliyotolewa na Azaki ya Tanzania Women Cross – Party Platform/ ULINGO.