Daily Archives: September 19, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 19 Septemba, 2021 amewasili nchini Marekani kuhudhuria Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Mara baada ya kuwasili Jijini New York, Mhe. Rais Samia amepokelewa na Watanzania wanaoishi nchini humo na kuwashukuru kwa mapokezi makubwa waliyomuonesha.

Mhe. Rais Samia amewafahamisha watanzania hao kuwa yeye na ujumbe wake mbali na kuhudhuria Mkutano huo pia atahudhuria mikutano mbalimbali itakayojali masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, usalama wa chakula na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 

Akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayoikumba dunia, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania haijaathirika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mataifa mengine kufuatia kuwepo kwa mipango mbalimbali ya kukabiliana na athari za mazingira nchini Tanzania.