Daily Archives: September 26, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi kama ifuatavyo:-

  • Amemteua Bw. Omari Issa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO.

Kabla ya uteuzi huu, Bw. Issa alikuwa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Utekelezaji wa Miradi (PDB).

  • Amemteua Bw. Maharage Chande kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO.

Kabla ya uteuzi huu, Bw. Chande alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Afrika Mashariki na Magharibi wa Multichoice Afrika.

Bw. Chande anachukua nafasi ya Dkt. Tito Mwinuka.

  • Amemteua Bw. Michael Minja kuwa Kamishna wa Petrol na Gesi, Wizara ya Nishati.

Kabla ya uteuzi huu Bw. Minja alikuwa mkurugenzi Mkuu – TIPPER.

  • Amemteua Bw. Felschemi Mramba kuwa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu.

Kabla ya uteuzi huu Bw. Mramba alikuwa Mshauri Mkuu wa Kiufundi (Chief Technical Advisor) – TANESCO training School

  • Amemteua Bw. Hassan Seif Said kuwa Mkurugenzi Mkuu, Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Kabla ya uteuzi huu Bw. Seif alikuwa Meneja wa Kanda Mwandamizi wa Kanda ya Mashariki TANESCO.

Bw. Said anachukua nafasi ya Bw. Amos Maganga.

Uteuzi huu umeanza tarehe 23 Septemba, 2021.

Wakati huohuo, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga amewahamisha Watumishi Waandamizi watano (5) toka TANESCO kwenda Ofisi ya Rais, Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambako watapangiwa kazi nyingine kama ifuatavyo:-

  1. Mhandisi Khalid James – Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uwekezaji.
  2. Mhandisi Raymond Seya – Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji na Masoko.
  3. Mhandisi Isaac Chanje – Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usafirishaji.
  4. Bw. Nyelu Mwamaja – Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi.
  5. Bw. Amos Ndegi – Mwanasheria wa TANESCO.  

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 25 Septemba, 2021 amerejea Jijini Dar es Salaam akitokea New York nchini Marekani alipokuwa akihudhuria Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Rais Samia amepokelewa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla, viongozi mbalimbali wa Vyama vya Siasa, viongozi wa dini pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam,

Wananchi hao wamesema wamejitokeza kwa wingi kumpokea Mhe. Rais Samia na kumpongeza kutokana na kuiwakilisha vyema Tanzania kupitia hotuba yake aliyoitoa tarehe 23 Septemba, 2021 katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Mhe. Rais Samia amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa niaba ya Watanzania wote kwa kujitokeza kwa wingi kumpokea na kueleza kuwa hotuba yake ilijikita katika mambo makuu manne.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na mataifa na wadau wengine duniani kutatua changamoto zinazoukabili ulimwengu.

Mhe. Rais Samia katika hotuba yake pia ameeleza jinsi Tanzania inavyoungana na mataifa mengine kupambana na ugonjwa wa Virusi vya Korona, (UVIKO 19), juhudi za Serikali katika kukuza uchumi na athari za mabadiliko ya Tabia Nchi.

Mhe. Rais Samia amewaomba Watanzania kuungana na kushirikiana kwa pamoja ili kuendelea kuijenga Tanzania madhubuti ambayo imejengwa kwa zaidi ya miaka 60.