Daily Archives: September 28, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO YA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 27 Agosti, 2021 amepokea Hati za Utambulisho wa Mabalozi wawili walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Mabalozi waliowasilisha Hati za Utambulisho ni Mhe. Zahra Ali Hassan Balozi wa  Somali na Mhe. Nabil Hajlaoui Balozi wa Ufaransa wote wakiwa na makazi yao hapa nchini.

Akizungumza mara baada ya kupokea hati hizo, Mhe. Rais Samia amewapongeza Mabalozi hao na kuwaomba kufikisha salamu zake kwa viongozi wakuu wa nchi zao na kusisitiza kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano na ushirikiano kwa manufaa ya pande zote.

Kwa upande wao Mabalozi hao wamempongeza Mhe. Rais Samia kwa utendaji mzuri na kumuahidi ushirikiano.

Mabalozi hao wameeleza kuwa mataifa yao yana dhamira ya dhati ya kuimarisha uhusiano katika sekta mbalimbali hususan biashara na uwekezaji.

Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia amemuapisha Mhe. Balozi Togolani Edriss Mavura kuwa Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini.

Pia, Mhe. Rais Samia amemuapisha Bw. Mathew Modest Kilama kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma.

Hafla hiyo ya uapisho ilioyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa wajumbe watatu (3) kujaza nafasi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kama ifuatavyo:-

  1. Bi Asina Abdillah Omar ameteuliwa kwa kipindi cha pili kuendelea na majukumu ya Tume,  baada ya kipindi chake cha kwanza kumalizika tarehe 15 Septemba, 2021.
  • Mhe. Magdalena Kamugisha Rwebangira, kutoka Chama cha Wanasheria (TLS).
  • Mhe. Jaji Jacob Mwambengele, Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Uteuzi huu umeanza tarehe 14 Septemba, 2021.