Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 28 Septemba, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Hafez Ghanem, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Rais Samia amemueleza Dkt. Ghanem vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita ambavyo ni kuboresha huduma za jamii ikiwemo elimu na afya pamoja na ujenzi wa miradi ya kimkakati.
Aidha, Mhe. Rais Samia amemueleza Dkt. Ghanem kuwa kwa sasa Serikali inapitia sera zake za kodi kwa majadiliano na wadau ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji katika kuimarisha sekta binafsi ili iweze kushindana na kuchangia ajira nchini.
Mhe. Rais Samia pia amezungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali kuweka taarifa na kuongeza ufanisi katika makusanyo kupitia matumizi ya TEHAMA.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Ghanem amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuendelea kushirikiana na Benki ya Dunia katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.
Aidha, Dkt. Ghanem ameeleza dhamira ya Benki ya Dunia ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuwajengea uwezo wanawake kiuchumi kuanzia wanapozaliwa, kimasomo na katika afya.
Pia, Dkt. Ghanem amesema Benki hiyo ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika ununuzi, usafirishaji na utoaji elimu ya UVIKO 19 kwa jamii ili kutoa muamko kwa wananchi kujitokeza kupata chanjo.