Daily Archives: October 13, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema uteuzi anaoufanya katika nafasi mbalimbali za uongozi katika Serikali anaufanya kwa kuzingatia uwezo wa mtu na si kwa kuangalia kabila la mtu au sehemu anapotoka.

Mhe. Rais Samia amesema hayo tarehe 11 Oktoba, 2021 wakati akizungumza mara baada ya kumuapisha Mhe. Sofia Edward Mjema (Mkuu wa mkoa wa Shinyanga), Mhe. Jaji Omar Othman Makungu (Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania) pamoja na Jaji Mustapha Siyani (Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania) katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma.

Amesema wapo baadhi ya watu ambao wanapoondolewa katika nafasi zao za uteuzi huona kuwa wametenguliwa kwa kigezo cha ukabila jambo ambalo si la kweli bali uteuzi anaoufanya unazingatia uwezo na utendaji kazi wa mtu husika. Hivyo kiongozi yeyote akifanya makosa ataondolewa katika nafasi yake bila kujali kabila lake.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kufanya kazi kwa kuzingatia viapo vyao na kuacha  tabia ya kujikweza na kujiingiza katika vitendo vya rushwa.

Mhe. Rais Samia pia amewataka Wakuu wa Mikoa kusimamia kwa umakini fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 zilizopelekwa katika mikoa yao na kuelekeza kuwa miradi hiyo inapaswa kutekelezwa ndani ya muda wa miezi 9 hivyo wahakikishe wanaisimamia vizuri kwa kuzingatia muda uliokusudiwa na kuendelea kukusanya kodi kama inavyotakiwa.

Kwa upande wa viongozi wa Mahakama aliowaapisha, Mhe. Rais Samia amewataka kujipanga vyema na kusimamia Mfumo wa Mtandao ili utumike katika utekelezaji majukumu yao kama alivyoagiza hapo awali.

Hafla hiyo ya kuwaapisha viongozi hao imehudhuriwa pia na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Naibu Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Akson, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Wakatihuohuo, Mhe. Rais Samia amepokea Hati ya Utambulisho kutoka kwa Mhe.  Chen Mingjian Balozi wa  Jamhuri ya Watu wa China hapa nchini.

Mhe. Rais Samia amempongeza Balozi huyo kwa kuteuliwa kuiwakilisha nchi yake na kumuahidi kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande  wa Balozi Mhe. Mingjian amempongeza  Mhe. Rais Samia kwa utendaji wake wa kazi na kumuahidi kuimarisha uhusiano katika sekta mbalimbali hususan biashara na uwekezaji.