Daily Archives: November 8, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 08 Novemba, 2021 amekutana na kuzungumza na Katibu Mtendaji wa African Leaders Malaria Alliance (ALMA), Bi. Joy Phumaphi, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Rais Samia amemshukuru Bi. Phumaphi na kumhakikishia ushirikiano wa Serikali katika kukabiliana na malaria nchini pamoja na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Mhe. Rais Samia amesema jitihada mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa  na Serikali, ikiwa ni pamoja na uundwaji wa Mabaraza ya Malaria ngazi zote pamoja na kupitia Umoja wa Wabunge wa Tanzania walio katika mapambano dhidi ya Malaria (TAPAMA) ambao wanafanya kazi kubwa ya kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika majimbo yao.

Aidha, Mhe. Rais Samia amemuomba Bi. Phumaphi kuisaidia Tanzania kupata teknolojia ya kisasa ili kuboresha vyandarua vinavyozalishwa nchini pamoja na kuwezesha viuadudu vya kibaiolojia kuweza kutambulika kimataifa ikiwa ni moja ya jitihada za kuwezesha Serikali kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa wa Malaria kufikia sifuri  ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa ALMA Bi. Phumaphi amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa ushirikiano wake na ALMA na kumpongeza kwa jitihada mbalimbali anazochukua kukabiliana na ugonjwa wa  Malaria nchini Tanzania.

Bi. Phumaphi amesema Tanzania ni mojawapo ya nchi za kuigwa Afrika kutokana na mafanikio iliyoyapata katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo, hivyo ALMA itaendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto mbalimbali.