Daily Archives: November 19, 2021

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Ahutubia Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hospitali ya Bugando Jijini Mwanza Tarehe 18 Novemba, 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikata utepe kuzindua rasmi huduma ya MRI katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hospitali ya Bugando Jijini Mwanza 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipata maelezo kuhusu utoaji wa huduma ya MRI mara baada ya kuzindua rasmi huduma hiyo kwenye Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hospitali ya Bugando Jijini Mwanza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwasili katika Viwanja vya Hospitali ya Bugando kwa ajili ya Jubilei ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hospitali ya Bugando Jijini Mwanza 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiondoa kitambaa kuzindua rasmi Mnara wa Kumbukumbu ya Jubilei  Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hospitali ya Bugando Jijini Mwanza 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Maaskofu wa Hospitali ya Bugando mara baada ya kuzindua rasmi Mnara wa Kumbukumbu ya Jubilei Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hospitali ya Bugando Jijini Mwanza 
.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia kwenye Jubilei ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hospitali ya Bugando Jijini Mwanza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiagana na kuzungumza na Viongozi na Vijana mbalimbali katika Uwanja wa ndege wa Mwanza baada ya kuhitimisha shuhuli ya uzinduzi wa Jubilei ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hospitali ya Bugando Jijini Mwanza
.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiangalia ngoma ya Bom inayochwezwa na Watoto wa chekechea mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar tarehe 18 Novemba, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Viongozi mbalimbali wa Serikali mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar tarehe 18 Novemba, 2021.
.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote na Kamati zao za Ulinzi na Usalama kuhakikisha wanaweka ulinzi kwenye vyanzo vyote vikuu vya maji na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaochepusha maji kwenye vyanzo hivyo.

Mhe. Rais Samia ametoa maagizo hayo tarehe 18 Novemba, 2021 wakati akihutubia kwenye Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Jijini Mwanza na kutaka agizo hilo kuanza kutekelezwa mara moja.

Amesema Serikali haiwezi kuweka rehani maisha ya watanzania walio wengi kwa manufaa ya watu wachache ambao wamekuwa wakihodhi maji ama kuharibu vyanzo vya maji kwa shughuli zao mbalimbali.

Mhe. Rais Samia ametaja sababu nyingine zinazosababisha uhaba wa maji nchini kuwa ni ukataji miti kiholela ambao kwa kiasi kikubwa unasababisha jangwa na kuchochea mabadiliko ya tabianchi.

Kuhusu Jubilei ya Miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Mhe. Rais Samia ameupongeza uongozi wa Hospitali hiyo kwa kuanzisha huduma ya matibabu ya Saratani ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Vilevile, Mhe. Rais Samia ameitaka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na  Hospitali ya Rufaa na Kanda Bugando kuendelea kufanya utafiti kama walivyoagizwa na mtangulizi wake ili kubaini sababu za kuwa na kiwango kikubwa cha saratani katika Kanda ya ziwa.

Mhe. Rais Samia amesisitiza kuwa tafiti hizo zijikite kwenye kubaini chanzo cha saratani na sababu zinazopelekea Kanda ya Ziwa kuongoza kuwa na waathirika wa saratani ambapo wanawake ndio wamekuwa wahanga wakubwa wa ugonjwa huo.

Ameongeza kuwa, uwepo wa Taasisi ya Saratani katika Hospitali ya Bugando imesaidia Serikali kupunguza gharama za safari ambazo zilikuwa zinagharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.9 kwa mwaka.

Awali, Mhe. Rais Samia amezindua mtambo wa kutoa huduma za MRI uliogharimu shilingi bilioni 2.4 kupitia mradi wa ushirika na Serikali ya Uholanzi.

Kuhusu matumizi sahihi ya fedha za mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani  (IMF), kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kukabiliana na madhara ya UVIKO19, Mhe. Rais Samia amesema ni vizuri ubora wa vifaa vitakavyonunuliwa ukazingatiwa na kuwataka wahusika kutojificha kwenye kivuli cha kipengele cha manunuzi cha single source kwa kutoa zabuni kwa kampuni zisizo na sifa na uzoefu.

Katika fedha hizo za mkopo kutoka IMF, Hospitali ya  Rufaa na Kanda Bugando imepata shilingi bilioni 4.2 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, huduma za dharura na huduma za wagonjwa mahututi.

Pia, katika maadhimisho hayo, viongozi wa dini wamefanya Sala na Dua kwa ajili ya kuliombea Taifa liweze kupata mvua za kutosha ili tuweze kukabiliana na hali ya hewa ya hivi sasa.

Mhe. Rais Samia amewasili Zanzibar na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Idrisa Kitwana, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Abdallah Sadallah Mabodi na viongozi wengine wa Chama na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.