Daily Archives: November 21, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 20 Novemba, 2021 ameshiriki Mkutano wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (AWLN) uliofanyika kwa njia ya mtandao, kujadili masuala ya kuwainua wanawake  kiuchumi katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Rais Samia amesema kupitia mkutano wao wa mwisho uliofanyika mwezi Mei mwaka 2021 kwa njia ya mtandao, umemsaidia katika utekelezaji wa baadhi ya majukumu yake ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa ajenda za maendeleo nchini Tanzania.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewafahamisha washiriki wa mkutano huo kuwa tayari ameshaanzisha Mabaraza ya kuwawezesha Wanawake kiuchumi katika ngazi mbalimbali nchini Tanzania ikiwa ni moja ya nguzo za mtandao huo.

Mhe. Rais Samia pia amethibitisha kushiriki kwa njia ya mtandao  Mkutano wa Viongozi Wanaume ulioitishwa na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mhe. Felex Tshisekedi utakaofanyika tarehe 25 Novemba, 2021.

Pia Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa viongozi hao kuendelea kutengeneza Sera na Mifumo ya Kisheria itakayowezesha wanawake kuinuliwa kiuchumi.

Mkutano huo pia umejadili na kukubaliana kuwa na mshikamano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili  wanawake katika maeneo yenye mgogoro Barani Afrika.

Mtandao wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (AWLN) unaongozwa na Nguzo sita zenye lengo la kuchochea Ajenda 2030 ya Umoja wa Mataifa na ile ya 2063 ya Umoja wa Afrika (AU).