Daily Archives: November 24, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 23 Novemba, 2021 amezindua Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa iliyofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.

Mhe. Rais Samia amesema jukumu la usalama barabarani sio la Askari wa barabarani peke yao bali  ni la kila mwananchi  katika jamii na hivyo kumtaka kila mwananchi kuwa makini na kuhakikisha matumizi sahihi ya barabara.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema suala la usalama barabarani lipewe uzito wa kuwa ajenda ya kitaifa katika majukwaa pamoja na kuwahusisha kikamilifu washirika wa maendeleo hasa wale ambao wamepiga hatua kubwa katika maendeleo ya nyanja ya usalama barabarani.

Mhe. Rais Samia amesema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa ajali za barabarani bado zimekuwa zikigharimu maisha ya watanzania wengi mbali na juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwekeza kwenye miundombinu bora ya barabara.

Vilevile, Mhe. Rais amesema vijana wengi ambao ndio nguvu kazi ya taifa wamekuwa wahanga wakubwa wa ajali za barabarani ambapo asilimia kubwa za ajali hizo husababishwa na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda.

Mhe. Rais Samia amesema takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano jumla ya wapanda pikipiki 2,220 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani na kusababisha majeruhi 4,202.

Mhe. Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuwa na msaada kwa wananchi na sio kero kwao ili kujenga mahusiano mazuri katika jamii hali itakayopelekea kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali kwa wakati.

Ametaja baadhi ya kero zinazofanywa na Askari wa usalama barabarani kuwa ni pamoja na kushikilia leseni za madereva kwa muda mrefu, kulazimisha madereva kulipa faini za papo kwa papo kinyume na ilivyo Sheria ya Usalama Barabarani, hivyo kuwataka wahusika kubalika mara moja.

Aidha, Mhe. Rais Samia ameliagiza Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikianana na vyuo vikuu, vyuo vya ufundi  na chuo cha Usafirishaji (NIT) kuwekeza katika utafiti wa suala la usalama barabarani ili kupata suluhu ya kisayansi na kimfumo ya namna ya kupunguza ajali za barabarani.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amelitaka Baraza la Usalama Barabarani kutumia mitandao ya kijamii kutoa elimu ya usalama barabarani kwasababu kwa hivi sasa dunia ni ya kidijitali na taarifa nyingi zipo kiganjani ambapo vijana wengi hutumia mitandao hiyo.

Pia, Mhe. Rais Samia ameelekeza kufanyika kwa ukaguzi wa kina wa magari kabla ya kutoa stika za usalama barabarani na kutaka Taasisi zinazohusika kukaa na wadau na Sekta binafsi kujadiliana jinsi ya kuendesha zoezi hilo kwa pamoja kwa kutumia vifaa vya kisasa.

Katika Maadhimisho hayo ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, Mhe. Rais Samia amekabidhi vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani vilivyotolewa na wadau mbalimbali. Pia, Mhe. Rais alitembelea mabanda mbalimbali pamoja na kupata maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na wadau mbalimbali kuhusu usalama barabarani.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Afungua Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha tarehe 23 Novemba 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwasili katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha kwa ajili ya kufungua Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipata maelezo kuhusu matumizi ya Barabara alipotembelea mabanda ya maonesho kwenye maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama yaliyofanyika leo tarehe 23 Novemba 2021 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.Wa pili kulia Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza jambo kwa Makamanda wa Jeshi la Polisi alipotembelea mabanda ya maonesho kwenye maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyoanza leo tarehe 23 Novemba 2021 katika Uwanja wa  Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawe.
Viongozi pamoja na Wananchi mbalimbali wa mkoa wa Arusha wakiwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuhudhuria Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani iliyoanza leo 23 Novemba 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikabidhi jumla ya Pikipiki 26 kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro kwa ajili ya kuongeza kasi ya kufanya Doria kwa Jeshi hilo, kwenye maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama yalioanza leo tarehe 23 Novemba 2021 katika Uwanja wa  Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha. Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe.  Khamis Hamza Chillo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizunguza na Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. George Simbachawene kushoto, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe.  Khamis Hamza Chillo na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro baada ya kufungua  maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyofanyika leo tarehe 23 Novemba 2021 katika Uwanja wa  Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia katika maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyoanza leo tarehe 23 Novemba 2021 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha Uwanja wa  Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
.
.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipata maelezo kuhusu matumizi ya Barabara na Madaraja pamoja na kuvuka katika maeneo hayo  kutoka kwa mtoto wa Shule ya msingi mkoani  Arusha alipotembelea mabanda ya maonesho kwenye maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyofanyika tarehe 23 Novemba, 2021 katika Uwanja wa  Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha. Wa pili kulia Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Dodoma wakati akitokea mkoani Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasili  katika Uwanja wa ndege wa Dodoma wakati akitokea mkoani Arusha.