Daily Archives: November 26, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uswisi Bi. Patricia Danzi leo tarehe 26 Novemba, 2021 Jijini Dodoma.

Katika Mazungumzo hayo, Bi. Danzi amempongeza Mhe. Rais Samia kwa maendeleo makubwa yaliyopatikana nchini Tanzania kwa kipindi kifupi tangu aingie madarakani ikiwa ni pamoja na Serikali kuruhusu watoto wa kike waliopata ujauzito kurudi shuleni.

Bi. Danzi amemueleza Mhe. Rais Samia kuwa Serikali ya Uswisi imekuwa na ushirikiano wa kimaendeleo na Serikali ya Tanzania kwa zaidi ya miaka 40  katika sekta za afya, elimu katika masuala ya utafiti na kuwawezesha vijana katika mipango mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia ameishukuru Serikali ya Uswisi kwa ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

Mhe. Rais Samia pia amemueleza Bi. Danzi hatua zinazo chukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha huduma za jamii kwa wananchi ikiwa ni pamoja na sekta ya elimu,  maji, afya na nyinginezo.

Kuhusu UVIKO 19, Mhe. Rais Samia amemueleza Bi. Danzi kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabilaiana na ugonjwa huo ikiwemo kutoa chanjo na elimu kwa wananchi katika ngazi mbalimbali.

Mhe. Rais Samia amewasili Jijini Dar es Salaam leo akitokea Jijini Dodoma.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Akutana na Kuzungumza na Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uswisi Jijini Dodoma leo tarehe 26 Novemba, 2021 ns Kurejea Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uswisi ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bi. Patricia Danzi, wakati ujumbe huo ulipofika Jijini Dodoma leo tarehe 26 Novemba, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uswisi ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bi. Patricia Danzi kushoto, wakati ujumbe huo ulipofika Jijini Dodoma leo tarehe 26 Novemba, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam akitokea mkoani Dodoma  leo tarehe 26 Novemba, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Viongozi mbalimbali wa Serikali alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam akitokea mkoani Dodoma  leo tarehe 26 Novemba, 2021.