Daily Archives: November 26, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 25 Novemba, 2021 amefungua Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha nchini na kueleza kuridhishwa kwake na ukuaji wa sekta ya fedha na nafasi yake katika uchumi wa Tanzania.

Mhe. Rais Samia ameeleza kuwa nchi yetu ikielekea kutimiza miaka 60 ya uhuru mafanikio mbalimbali yamepatikana katika sekta ya fedha na kupelekea Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 barani Afrika ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi.

Katika mafaniko hayo ndani ya miaka 60, Mhe. Rais Samia amesema mafanikio mengine ni ukuaji endelevu wa uchumi , utulivu  wa bei za bidhaa na huduma pamoja na utulivu katika mwenendo wa thamani ya fedha yetu dhidi ya fedha za kigeni

Aidha, Mhe. Rais amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla ambapo hivi sasa mauzo ya Dhamana za Serikali yamekuwa na uhitaji mkubwa kuliko upatikanaji wake na hicho ni kiashiria kikubwa cha muamko wa sekta binafsi katika kushirikiana na Serikali kutekeleza wajibu wake.

Mhe. Rais Samia amesema hali ya umasikini imepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2015 hadi asilimia 26.2 kwa mwaka 2020  na umri wa kuishi kuongezeka kutoka miaka 50 hadi miaka  66.

Mhe. Rais Samia amesema pia nchi yetu imepiga hatua kubwa kimaendeleo na kufikia kuwa nchi ya kipato cha kati mwezi Julai 2020 hivyo tutahakikisha sera zetu zinakwenda kukuza uchumi ili tusirudi nyuma.

Aidha. Mhe. Rais Samia amesema licha ya UVIKO 19 kuathiri uchumi wetu hasa katika sekta ya utalii, Serikali imejitahidi kupambana na athari hizo na kuhakikisha uchumi wetu hauathiriki kwa kiasi kikubwa na kuwapa nafasi wananchi kufanya kazi za uzalishaji tofauti na nchi nyingine zilizoweka zuio la kutoka nje.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kupambana na kuzuia athari za janga la UVIKO 19 zisitupate kwa kiwango kikubwa kwa kuleta chanjo ambayo mpaka hivi sasa wananchi wanaendelea kupatiwa.

Mhe. Rais Samia amesema ana matumaini kuwa kutokana na athari mbalimbali za ugonjwa huo kwenye uchumi mkutano huo utakuja na suluhisho yatakayoweza kusaidia uchumi wa Tanzania kuzidi kukuwa.

Aidha, Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa Serikali iliwasiliana na Taasisi mbalimbali za fedha duniani kuhusu  msamaha wa madeni au kurefusha muda wa ulipaji wa madeni hayo kutokana na UVIKO 19 kuathiri uchumi wetu. Pia, Serikali ilipata mkopo ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na athari hizo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka washiriki wa Mkutano huo kuja na mapendekezo ya namna bora ambayo teknolojia inaweza kusaidia ukuaji wa sekta ya fedha na pia kutathmini matumizi ya sarafu za mtandaoni (crypto currencies) ambazo zinaendelea kuenea duniani ili Tanzania iwe mshiriki mzuri katika nyanja hizo.

Mhe. Rais Samia ametoa wito pia kwa Taasisi za fedha nchini kupunguza kiwango cha riba wanachotoza katika mikopo ili watu wengi zaidi waweze kupata mikopo himilivu kwa ustawi wa uchumi wa

Taifa na kutoa fursa bora zaidi kwa sekta binafsi kuweza kufanya biashara.