Daily Archives: December 7, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 06 Desemba, 2021 amezindua kiwanda cha kutengeneza vifaa vya umeme cha Elsewedy (Elsewedy Electric East Africa Ltd), kilichopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam.

Ufunguzi wa Kiwanda hicho ni Sehemu ya maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru ambapo Mhe. Rais anaweka Mawe ya Msingi na kufungua Miradi mbalimbali ya Maendeleo.

Mhe. Rais Samia amesema uwekezaji wa Kiwanda hicho ni kielelezo kuwa nchi ipo katika njia sahihi ya kujikomboa kiuchumi, kuondoka katika utegemezi wa kuagiza bidhaa kutoka nje kama ilivyodhamiria wakati nchi ikipata uhuru miaka 60 iliyopita.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Kiwanda hicho ambacho kitakuwa na uwezo kwa kuzalisha tani 15,000 za nyaya za umeme, transfoma 1,500 na mita 100,000 za umeme kwa mwaka zitakazotumika nchini na kuondoa utegemezi wa kununua bidhaa hizo nje ya nchi na nusu ya bidhaa hizo zitauzwa katika masoko ya nje na kuongeza fedha za kigeni.

Mhe. Rais Samia ameziagiza Wizara na Taasisi zinazohusika na masuala ya uwekezaji kuhakikisha zina wawezesha na kuweka mazingira mazuri katika sekta hiyo badala ya kuwawekea vikwazo na kuwakatisha tamaa.

Pia, Mhe. Rais Samia amewahakikishia wawekezaji zaidi ya 100 kutoka nchini Misri kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini pamoja na mitaji na soko kwa bidhaa watakazozalisha ikiwemo uwepo wa rasilimali watu wenye uzoefu kwa ajili ya kutumika kwenye uwekezaji wao.

Mhe. Rais Samia ameagiza Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kujenga ushirikiano na Kituo cha Uwekezaji cha Misri ili kujifunza mazuri kutoka kwao kwa lengo la kuboresha kama alivyojionea utendaji kazi wa Kituo hicho cha nchini Misri wakati alipofanya ziara nchini humo.

Vilevile, Mhe. Rais amewataka watendaji wa Serikali wanaohusika kuhakikisha wanakamilisha taratibu za upatikanaji wa ardhi katika eneo hilo kwa kuzingatia sheria ili wawekezaji hao waendelee na ujenzi wa mji wa viwanda ambao unatarajiwa kutoa ajira na kuchangia uchumi wa nchi.  

Akiwa njiani kuelekea kiwandani hapo, Mhe. Rais Samia alipata fursa ya kuwasalimia wananchi wa Kibada Wilayani Kigamboni na kuwaahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo changamoto ya maji, umeme na barabara.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia amemuapisha Profesa Adelardus Lubango Kilangi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil na kumtaka kutumia fursa za uwekezaji zilizopo nchini humo katika sekta za kilimo, utalii na michezo ili kuinufaisha Tanzania kupiga hatua zaidi katika maendeleo.