Daily Archives: December 11, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta ameendelea na Ziara yake ya Kiserikali ya siku mbili hapa nchini, ambapo tarehe 10 Desemba, 2021 amepokelewa rasmi na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Mara baada ya kuwasili, Mhe. Rais Kenyatta amekagua gwaride lililoandaliwa kwa heshma yake na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kupigiwa mizinga 21.

Mhe. Rais Kenyatta na Mwenyeji wake Mhe. Rais Samia wamefanya mazungumzo rasmi yaliyohusu kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya.

Wakizungumza na vyombo vya habari kuhusu ziara hiyo, Mhe. Rais Samia amesema ziara ya Mhe. Rais Uhuru Kenyatta inafuatia mualiko wake aliompa wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia nchini Kenya mwezi Mei mwaka huu.

Mhe. Rais Samia amesema katika mazungumzo yao pia wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika biashara kwa kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Kenya kimezidi kuongezeka kutoka shilingi bilioni 885.4 mwaka 2013 hadi kufikia shilingi Trilioni 1.1 mwaka 2020.

Mhe. Rais Samia amesema wakati wa ziara yake nchini Kenya walikubaliana na Mhe. Rais Kenyatta kuondoa vikwazo visivyokuwa vya kikodi ambapo hadi sasa jumla ya vikwazo 46 kati ya 64 vilivyokuwepo vimeondolewa.

Kuhusu zoezi la kuimarishwa mpaka kati ya Tanzania na Kenya, Mhe. Rais Samia amewataka Mawaziri wanaohusika kufanyia kazi suala hilo ili liweze kukamilika.

Mhe. Rais Samia amezungumzia makubaliano ya pamoja katika kukabiliana na UVIKO 19 kwa kuwataka Mawaziri husika kushirikiana kwa pamoja katika kukabiliana na tatizo hilo.

Marais hao pia wamezungumzia kushirikiana katika sekta ya utalii kwa kuungana katika kuuza vivutio vya utalii katika nchi zao kwa manufaa ya pande zote mbili na kukabiliana kwa pamoja kutatua changamoto zinazojitokeza.

Mhe. Rais Samia amemkabidhi Mhe. Rais Kenyatta cheti cha umiliki wa wanyama pori 20 aina ya Korongo ambapo Rais huyo wa Kenya nae ameridhia ombi la Tanzania kuipatia majike ya Faru weusi.

Mhe. Rais Samia na Mhe. Rais Kenyatta wameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano kuhusu masuala ya Uhamiaji, Hati ya Makubaliano kuhusu masuala ya Magereza, Hati ya Makubaliano kuhusu udhibiti wa magonjwa ya mifugo mipakani, Hati ya Makubaliano kuhusu masuala ya afya, Hati ya Makubaliano kuhusu masuala ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkataba wa kubadilishana wafungwa na Hati ya Makubaliano ya masuala ya Uwekezaji.

Kuhusu Ujenzi wa barabara katika ukanda wa Pwani ya Tanzania na Kenya (Bagamoyo-Malindi), Mhe. Rais Samia na Mhe. Rais Kenyatta wamekubaliana kufungua ukanda huo kwa kuunganisha kwa ujenzi wa barabara ya lami ili wananchi wa pande husika waweze kufaidi matunda ya maendeleo kama sehemu nyingine.

Kwa upande wake Mhe. Rais Uhuru Kenyatta amemshukuru Mhe. Rais Samia pamoja na watanzania kwa kumualika kuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru ambayo yana historia kubwa kwake.

Mhe. Rais Kenyatta amesisitiza kuendelea kushirikiana na kutafuta mbinu mbalimbali ambazo zitawezesha nchi zetu mbili kuwa karibu kindugu, kibiashara na kiutalii kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote.

Kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa nchini Kenya, Mhe Rais Samia amesema suala hilo wamewaachia Mawaziri wa Nishati walishughulikie ili kusaidia mradi huo uanze mara moja.

Mhe. Rais Samia ameagana na mgeni wake Mhe. Kenyatta katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini                 Dar es Salaam.