Daily Archives: December 12, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 11 Desemba, 2021 amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Mhe. Moussa Faki Mahamat, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika mzungumzo hayo, Mhe. Faki amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa mualiko wa kuhudhuria sherehe za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru.

Mhe. Faki amesema anategemea kuwa kama Tanzania ilivyokuwa kinara kwenye ukombozi wa Afrika basi itakuwa kinara pia katika kuchangamkia fursa ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) katika kukuza biashara ikizingatiwa kuwa Tanzania kupitia miundombinu yake ya bandari imeweza kurahisisha biashara kwa nchi jirani zinazotumia bandari hiyo.

Amesema Tanzania ni kitovu muhimu cha kuunganisha nchi jirani kibiashara na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali katika nchi hizo kutokana na jiografia yake.

Pia, Mhe. Faki amempongeza Mhe. Rais Samia kwa uongozi wake tangu aingie madarakani na jitihada zake za kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia amemshukuru Mhe. Faki kwa kuhudhuria sherehe za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru na kukutana nae kumueleza mambo mbalimbali yanayoendelea Barani Afrika na changamoto zake.

Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Faki kwa kuchaguliwa kwa muhula wa pili kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika.

Aidha, Mhe. Rais Samia amemueleza Mhe. Faki kuwa Tanzania haikuachwa nyuma na athari za UVIKO 19 kiuchumi, lakini inajitahidi kukabiliana na athari hizo kupitia njia mbalimbali ili kuhakikisha uchumi wake unaimarika.

Mhe. Rais Samia amesema ni wakati sasa kwa nchi za Afrika kutumia fursa zilizopo baada ya athari za UVIKO 19 kujiimarisha kiuchumi kwasababu nchi hizo zina fursa nyingi kiuchumi.