Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema ameamua kuiondoa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe 16 Desemba, 2021 wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kuhusu Kizazi chenye Usawa, Jijini Dodoma.
Pia, Mhe. Rais Samia amesema Wizara ya Afya ina mambo mengi hivyo ni muhimu kuitenga kwasababu sekta ya afya peke yake inachukua sura kubwa ya wizara, hivyo ikitenganishwa itafanya kazi zake vizuri na kupitia hilo atamshauri Rais wa Zanzibar naye afanye mabadiliko hayo.
Akizungumza kuhusu Jukwaa la sasa la Kizazi chenye Usawa, Mhe. Rais Samia amesema kuwa huo ni mwendelezo wa jitihada mbalimbali zinazofanywa na Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma kimaendeleo pamoja na kuhakikisha lengo namba 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake na Wasichana).
Mhe. Rais Samia amesema wanawake ambao wanafikia asilimia 50 ya nguvu kazi ya taifa bado ni waathirika wakuu wa mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yanayoendelea katika maeneo mbalimbali.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema licha ya kuwa Wanawake ni washirika muhimu katika kufanikisha Malengo ya dunia kama vile kutokomeza njaa, afya na elimu bora, maji safi na salama, usafi wa mazingira na ukuaji wa uchumi bado kwa kiasi kikubwa ukuaji wao kiuchumi, kijamii na kisiasa haujawekwa vyema kwenye mipango mbalimbali ya Maendeleo na inapowekwa haitekelezwi ipasavyo.
Pia, Mhe. Rais Samia amesema pamoja na kuwa nusu ya sehemu ya watu duniani ni wanawake, lakini bado sehemu kubwa ya dunia haijatoa nafasi stahiki kuitumia ipaswavyo nguvu kazi ya wanawake. Pia amebainisha kuwa iwapo wanawake watatumiwa kikamilifu wana uwezo wa kuchangia uchumi wa dunia kwa takriban dola trilioni 28 kwa mwaka.
Mhe. Rais Samia amesema Serikali imeridhia na inatekeleza Mikataba na Maazimio ya Kikanda na Kimataifa ikiwemo Mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi kwa wanawake wa mwaka 1978, Azimio la Beijing la mwaka 1995, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030, Ajenda ya Maendeleo ya Afrika Tuitakayo ya 2063 ili kuleta ustawi wa wanawake na watoto na kuweza kunyanyua hadhi ya uchumi wa taifa letu.
Aidha, Mhe. Rais Samia ameziagiza sekta zote kupitia Wizara, Taasisi, Mashirika, Wakala na Halmashauri kulipa kipaumbele suala la utekelezaji wa ahadi zilizowekwa katika utekelezaji wa Jukwaa la usawa wa kijinsia kwa kuweka mikakati na bajeti ili kuweza kutekeleza na kufikia ahadi hizo.
Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa kila Wizara, Taasisi na Wakala wa Serikali kuhakikisha kuwa Maafisa wa jinsia wanajengewa uwezo na kupatiwa rasilimali zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao na kutekeleza ahadi za nchi.
Vile vile, Mhe. Rais Samia amewataka wadau wa maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia, UN Women pamoja na Balozi za hapa nchini ambazo zilishiriki Mkutano wa Paris na kuweka ahadi zao kidunia kutekeleza ahadi ya haki za usawa ikiwemo Canada, Ufaransa, Finland, na Taasisi mbalimbali kuisaidia Tanzania na kuiunga mkono katika kutoa rasilimali fedha na utaalamu katika utekelezaji wa Mpango huu ili kuhakikisha ahadi tulizozitoa zinafikiwa.