Daily Archives: January 5, 2022

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kukopa mikopo yenye tija ili kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo itawanufaisha wananchi na kuwaletea maendeleo.

Mhe Rais Samia amesema hayo leo tarehe 04 Januari, 2022, mara baada ya kupokea taarifa za Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19, uliotokana na mkopo usio na riba wenye thamani ya shilingi Trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), katika hafla iliyofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema anawashangaa wanasiasa wachache wanaobeza jitihada za Serikali katika uchukuaji wa mikopo pamoja na ukusanyaji wa fedha za tozo na kusema hakuna taifa lolote duniani lililoendelea bila kufanya vitu hivyo na mpango huo utaendelea kama kawaida.

Mhe. Rais Samia amesema dhana ya kukopa haikuanza katika awamu hii ya Sita bali ilianza tangu nchi yetu ilipopata Uhuru na maendeleo yaliyopatikana katika awamu zote mengi yametokana na faida za kukopa.

Amesema atajitahidi kutumia kila fursa atakayoiona inafaa kuleta maendeleo kwa wananchi kama alivyoahidi wakati akila kiapo cha kushika madaraka na hafanyi hivyo kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2025.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka Mawaziri na Makatibu Wakuu kumuunga mkono na kuhakikisha wanasimamia fedha za miradi kama inavyotakiwa na kutoa taarifa kila wakati ili kwa wananchi waweze kujua kinachoendelea katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Mhe. Rais Samia amesema fedha hizo ziligawanywa katika maeneo ya Maji, Afya, Elimu, Uwezeshaji wa Wajasiriamali (vijana, wanawake na wenye ulemavu) na Mpango wa kuziwezesha kaya maskini (TASAF).

Pia Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa kiasi kingine cha fedha zilipangiwa kutumika katika kuchochea ukuaji wa Sekta ya Utalii na shughuli za uratibu na usimamizi (monitoring and evaluation) kwa Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pia ilinufaika na Mpango huu.

Kwa upande wa sekta ya Elimu, Mhe. Rais Samia amesema kuwa, licha ya mafanikio yaliyofikiwa ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, idadi ya watoto walioandikishwa kuanza elimu ya awali na msingi bado ni ndogo na kuwa haridhishwi na takwimu za uandikishaji wa wanafunzi wapya wa darasa la awali na darasa la kwanza.

Mhe. Rais Samia ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha kuwa wanahamasisha jamii ili watoto wenye umri na sifa za kuanza shule waweze kuandikishwa na kuanza masomo ifikapo tarehe 17 Januari, 2022 ambapo hadi sasa Ujenzi wa vyumba vya madarasa nchini umekamilika kwa asilimia 95.

Kwa upande wa sekta ya Afya, Mhe. Rais Samia ameitaka Wizara ya Afya kuhakikisha wanatoa mafunzo ya utumiaji na utunzaji wa vifaa vya kisasa vilivyoagizwa huku wakizingatia thamani ya fedha na ubora wa vifaa hivyo.  

Mhe. Rais Samia amewataka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kutumia fedha walizopewa kujenga barabara za kokoto na kuwataka TAMISEMI kujifunza teknolojia ya ujenzi wa barabara zinazodumu kwa maiaka 20 kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Aidha, Mhe. Rais Samia amelitaka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kusambaza umeme kwa wananchi kulingana na gharama halisi za upatikanaji wa nishati hiyo.