Daily Archives: January 11, 2022

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila kufuatia vifo vya watu 14, wakiwemo waandishi wa habari 6 waliofariki katika ajali ya barabarani iliyotokea leo tarehe 11 Januari, 2022 katika Kijiji cha Kalemela, Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.

Mhe. Rais Samia ametoa salamu hizo tarehe 11 Januari, 2022 wakati akizindua Kiwanda cha Nguo cha Basra Textile Mills Ltd kilichopo Chumbuni, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu ACP Blasius Chatanda amesema ajali hiyo iliyotokea katika barabara kuu ya Mwanza – Musoma ilihusisha gari aina ya Hiace iliyogongana na gari aina ya Landcruiser iliyokuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Gabriel aliyekuwa katika safari ya kikazi kuelekea Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka Wakuu hao wa Mikoa kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote, ndugu, jamaa, marafiki na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Akiwa katika eneo la Mkutano katika Kiwanda hicho cha Nguo cha Basra Textile Mills Ltd, Mhe. Rais Samia, viongozi mbalimbali pamoja na wananchi waliohudhuria sherehe za uzinduzi huo walisimama kimya kwa dakika moja kuwaombea marehemu wote waliofariki katika ajali hiyo.

Mara baada ya kutoa salamu hizo za pole, Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa vyuo vya mafunzo ya amali nchini kuendelea kuwajengea uwezo vijana wa kitanzania na wanawake kuwa wabunifu katika tasnia ya ushonaji nguo ili waweze kushindana katika soko la dunia.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema uzoefu unaonesha kuwa viwanda vingi vya ushonaji huajiri zaidi wanawake hivyo ni matarajio yake kuwa katika siku zijazo nchi yetu itasafirisha zaidi bidhaa za nguo nje ya nchi.

Mhe. Rais Samia amesema ujenzi wa Mradi huo wa kiwanda cha nguo ambao unatekelezwa kwa awamu tatu na mojawapo ikiwa ni uchakataji wa pamba utakuwa mkombozi katika kuleta ajira kwa vijana pamoja na wakulima wa zao hilo linalolimwa kwenye baadhi ya mikoa hapa nchini.

Mhe. Rais Samia amewaomba wawekezaji wa Kiwanda cha Basra kuharakisha uwekezaji katika hatua zilizosalia ili kilete tija na kuwezesha nchi kuacha kuagiza vitambaa na nguo kutoka nje ilhali malighafi zote za kuzalisha nguo zinapatikana hapa nchini.

Mhe. Rais Samia pia amewataka wawekezaji kutumia fursa ya kufanya biashara katika Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) kwa kuwa Tanzania imeridhia Itifaki ya kujiunga na soko hilo.

Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa vijana watakao ajiriwa katika Kiwanda cha Basra wafanye kazi kwa bidii, uadilifu, weledi na uaminifu na kutambua kuwa biashara ya sasa inakabiliwa na ushindani mkubwa duniani kote ambapo mzunguko wa bidhaa hauna mipaka.

Kwa upande mwingine, Mhe. Rais Samia amewataka wawekezaji wazingatie maslahi na haki za wafanyakazi wake ili kila mmoja aweze  kutekeleza wajibu na majukumu yake kikamilifu, kulipa kodi bila shuruti na kufuata sheria za nchi.

Mhe. Rais Samia amesema Mradi wa Kiwanda hicho umepewa hadhi ya Mradi mkakati hivyo amewataka pande zote mbili za Bara na Zanzibar kukaa pamoja na kutatua changamoto kwa kuondoa vikwazo vya kibiashara.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka wananchi kuendelea kulinda na kutunza amani iliyopo nchini ili kuweza kuwavutia zaidi wawekezaji na kufanikiwa katika kufikia malengo yetu.

UTEUZI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemteua Mhifadhi William Simon Mwakilema kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Kabla ya uteuzi huo, Mhifadhi Mwakilema alikuwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Mhifadhi Mwakilema anachukua nafasi ya Dkt. Allan Herbert Kijazi ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Uteuzi huu umeanza tarehe 08 Januari, 2022.