RAIS SAMIA AWAHIMIZA MAKATIBU MAHSUSI KUTUNZA SIRI ZA SERIKALI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Makatibu Mahsusi, Watunza Kumbukumbu pamoja na maafisa Utumishi kutunza siri za Serikali.
Rais Samia ametoa wito huo leo wakati akifungua Mkutano wa Tisa (09) wa Kitaaluma wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA).
Aidha, Rais Samia amesema suala la utunzaji wa siri za Serikali linasaidia kuepuka madhara yanayoweza kuwapata watu binafsi, Taasisi, Serikali na usalama wa Taifa letu.
Rais Samia pia amesema weledi, uaminifu, uadilifu na uzalendo ndiyo njia pekee itakayowafanya Makatibu Mahsusi kuaminiwa, kutegemewa na kuwawezesha kusonga mbele katika majukumu yao.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameridhia Chuo cha Utumishi wa Umma Tabora kuwa maalum kwa ajili ya mafunzo ya uhazili kwa ngazi zote ili kuzalisha Makatibu Mahsusi ambao watakwenda kutumika katika Taasisi za Serikali.
Halikadhalika, Rais Samia amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundo mbalimbali ya kada za kiutumishi, na maslahi ya watumishi wa umma kwa ujumla.