Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kufanya mabadiliko katika mitaala ya elimu (syllabus).
Rais Samia ametoa wito huo leo wakati akizindua Taasisi ya Wanawake Initiatives Foundation (MIF) na kueleza kuwa Zanzibar inakabiliwa na changamoto nyingi katika sekta ya Elimu.
Aidha, Rais Samia ametaka pia kuwepo na umakini katika sifa za walimu wanaoajiriwa, utungaji wa mitihani pamoja na uwezeshwaji wa vitendea kazi kwa wakaguzi.
Rais Samia amesema licha ya ufaulu kupanda kiasi kwa mwaka 2021 na kupungua kwa idadi ya waliopata sifuri, bado iko haja kwa Wizara hiyo pamoja na wadau kutafuta ufumbuzi wa kutatua changamoto zilizopo.
Rais Samia pia amewataka wazazi, walezi na jamii kubeba jukumu la kuhakikisha watoto wanahudhuria masomo ipasavyo na kuhakikisha kuwa wanapata muda wa kujisomea.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ameishukuru taasisi ya MIF kwa mchango na jitihada inazofanya katika kuinua kiwango cha elimu kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Rais Samia ametoa wito kwa Taasisi zingine zisizo za Serikali kuiga mfano wa MIF na kujitolea katika masuala ya kijamii hasa kwenye sekta ya elimu na malezi kwa watoto.