Monthly Archives: September 2023

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AENDELEA NA ZIARA YAKE MKOANI LINDI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema serikali inatarajia kujenga kiwanda cha ukubwa wa kati cha kubangua korosho.

Rais Samia amesema hayo leo wakati akihutubia wananchi wa Ruangwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kilimahewa.

Aidha, Rais Samia amesema lengo la kujenga kiwanda hicho ni kuwawezesha wananchi kuzalisha mafuta kwa kutumia maganda ya korosho ili waweze kupata faida zaidi na kuifanya Lindi ifunguke kiuchumi.

Vile vile, Rais Samia amesema serikali itaendeleza utafiti zaidi katika sekta ya madini ili kujua kiasi cha dhahabu kilichopo na kuwapanga wachimbaji wadogo wadogo ili wachimbe kitaalamu.  

Akizungumza na wananchi mara baada ya kuweka jiwe la msingi barabara ya Ruangwa – Nanganga (km 53.3) yenye thamani ya shilingi bilioni 50.3, Rais Samia amesema serikali ina mpango wa kuunganisha wilaya za mkoa wa Lindi kwa lami.

Mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi kwenye ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Mtama, Rais Samia amezungumza na wananchi na kuwataka kuongeza uzalishaji wa mbaazi na ufuta.

Rais Samia amezungumza na wananchi wa vijiji vya Nanganga na Nandagala akiwa njiani kuelekea Lindi mjini.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS SAMIA AHITIMISHA ZIARA YA KIKAZI MKOANI MTWARA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi kuacha kuwanyonya wakulima kwa kuwakata fedha za mauzo na kuzipeleka katika mifuko ya maendeleo ambayo haipo kisheria.

Rais Samia ametoa tamko hilo wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Bomani uliopo Masasi Mji.

Aidha, Rais Samia amewaelekeza viongozi hao kuiweka bayana mifuko iliyopo katika maeneo yao ili ijulikane, ikaguliwe na kuweka wazi mapato na matumizi yake.

Vile vile, Rais Samia amewataka watendaji wa Halmashauri ya Mji wa Masasi kuelekeza fedha za mapato ya halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo badala ya kusubiri fedha kutoka serikali kuu.

Kuhusu changamoto ya umeme katika Wilaya hiyo, Rais Samia amesema mkandarasi yuko kazini kuunganisha Masasi na gridi ya taifa na mradi huo unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 18 hivyo kufanya umeme kuwa wa uhakika.

Awali Rais Samia alikagua ghala la kuhifadhi chakula la Mangaka wilayani Nanyumbu na kuzungumza na wananchi wa eneo la Round About ambapo amewaeleza kuwa Serikani inatarajia kujenga kongani ya viwanda wilayani humo.

Rais Samia amehitimisha ziara yake mkoani Mtwara na kuanza ziara katika mkoa wa Lindi ambapo amehutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Likongolewe wilaya ya Liwale na Nachingwea mjini.