TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 14 Juni, 2021 amekagua ujenzi wa daraja la JPM, amezindua Mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira na ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Mwanza – Isakakatika siku ya 2 ya ziara yake Mkoani Mwanza.

Akizungumza na wananchi mara baada ya ukaguzi wa daraja la JPM linalojengwa katika eneo la Kigongo–Busisi, Mhe.Rais Samia amesema ujenzi wa daraja hilo ni sehemu ya mipango ya Serikali ya kulifanya Jiji la Mwanza kuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Maziwa Makuu.

Mhe. Rais Samia amesema daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.2 ambalo litagharimu shilingi Bilioni 716 litakapokamilika litafungua fursa zaidi za  kiuchumi kwa kuwawezesha wananchi hususani wafanyabiashara kuvuka kwa muda mfupi tofauti na ilivyo sasa ambapo hutumia muda mwingi kusubiri kivuko kwa ajili ya kuvusha bidhaa zao.

Akijibu ombi la Mbunge wa Jimbo la Sengerema Mhe. Hamisi Tabasam kuhusu ubadhirifu wa fedha katika Halmashjauri yao, Mhe. Rais Samia amesema Serikali imepeleka wakaguzi maalum kwa ajili ya kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali za kifedha zinazoikabili Halmashauri hiyo.

Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi wa maji katika eneo la Misungwi Mhe. Rais amesema mradi huo unaohusisha miji ya Magu na Lamadi na uliogharimu shilingi bilioni 45. 57 utawahudumia wananchi zaidi ya 64,000.

Mhe. Rais Samia ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha miradi yote ya maji inatekelezwa kwa wakati ili kufikia lengo la Serikali la kuwaondolea wananchi adha ya upatikanaji wa maji.

Mbali na wito huo, Mhe. Rais pia amewataka wana Misungwi na Watanzania kwa ujumla kuvitunza vyanzo vya maji ili kuendelea kupata majisafi na salama.

Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Mwanza – Isaka yenye urefu wa kilometa 341, utakaogharimu shilingi Trilioni 3.06,  amesema mradi huo utaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kusafirisha kwa haraka na kwa kiwango kikubwa cha mizigo na watu tofauti na ilivyo sasa.

Amesema mradi huu ni sehemu ya mradi mkubwa wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,605 ambao utatengeneza ajira 11,000 hivyo kuwataka wana Mwanza kuchangamkia fursa ya ujenzi wa reli hiyo.

Aidha amesema reli hiyo itapunguza muda wa kusafiri kati ya Mwanza hadi Dar es Salaam kutoka saa 17 za sasa kwa usafiri wa mabasi hadi saa 8 mradi utakapokamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *